NEWS

Wednesday 2 December 2020

Chandi ammiminia pongezi Rais Magufuli

Chandi Marwa


MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Chandi Marwa, amemmiminia Rais Dkt John Magufuli sifa akisema ni kiongozi mwenye utashi na shauku kubwa wa maendeleo ya wananchi kuwahi kutokea nchini.

 

“Binafsi ninapenda kuona Rais huyu akiendelea kuongoza Tanzania hata baada ya mwaka 2025,” amesema Chandi katika mahojiano na Mara Online News mjini Mugumu – Serengeti, hivi karibuni.

 

Ametaja mojawapo ya miradi mikubwa ya maendeleo inayokusudiwa kutekelezwa wilayani Serengeti chini ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli kuwa ni ujenzi wa uwanja wa ndege wenye hadhi ya kati – nje kidogo ya mji wa Mugumu.

Tembo wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayopakana na wilaya ya Serengeti

 

“Wana-Serengeti tuna matumaini makubwa ya kujengewa uwanja huo maana tayari TANAPA (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) wamekubali na Halmashauri yetu ya Wilaya kufanikisha ujenzi wake.

 

“Pia tayari tathmini imeshafanyika, wananchi wameshalipwa fidia ili kupisha ujenzi wa uwanja huo na vibali vimeshatolewa na mamlaka husika,” amesema Chandi.

Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayopakana na wilaya ya Serengeti

 

Hata hivyo, kada huyo wa CCM amesema mbunge na madiwani wana nafasi kubwa ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kuongeza fursa za uchumi na ajira kwa wananchi wilayani Serengeti.

 

“Faida za ujenzi wa uwanja huo ni pamoja na kuwezesha ndege zinazobeba watalii kutua huku Mugumu badala ya kutua na kubughudhi wanyamapori ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lakini pia utahamasisha shughuli za uwekezaji wa kitalii wilayani hapa,” amesema.

 

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Serengeti, Jacob Begha, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kutekeleza Ilani ya chama hicho tawala yenye vipaumbele vya kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Jacob Begha


“Ninampongeza sana Rais Magufuli kwa utendaji wake unaogusa moja kwa moja kero za wananchi, hasa wanyonge. Huku Serengeti tuna imani kubwa kwamba serikali yake itatutatulia migogoro ya binadamu na wanyamapori.

 

“Tuna imani kubwa pia kwamba serikali hii inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Magufuli itatekeleza ujenzi wa barabara ya Mugumu – Arusha na ile ya kutoka Butiama – Sanzake – Natta hadi Mugumu kwa kiwango cha lami.

 

“Lakini pia ninaipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuweka mikakati ya kuboresha bwawa la Manchira kwa kulijengea chujio la maji ili kuwezesha wakazi wa mji wa Mugumu na maeneo mengine kupata maji safi,” amesema Begha.

Pundamilia na nyumbu wakinywa maji ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inayopakana na wilaya ya Serengeti

 

Mwenyekiti huyo wa CCM alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa mbunge na madiwani kujenga mshikamano wa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa manufaa ya wananchi wa Serengeti na Taifa.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages