NEWS

Wednesday 30 December 2020

Katibu Mkuu TAMISEMI afurahishwa ukarabati Sekondari ya Tarime

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga (mwenye suti ya bluu) na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tarime, Mwalimu Machota Edward Kora (mwenye suti nyeusi), wakifurahia kazi nzuri ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo, jana Desemba 30, 2020.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga, ameelezea kuridhishwa kwake na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya Shule ya Sekondari ya Tarime mkoani Mara.

 

Nyamhanga amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ukarabati huo jana Desemba 30, 2020 na kuupongeza uongozi wa shule hiyo na Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa kusimamia vizuri kazi hiyo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga (mwenye suti mbele) na msafara wake wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Tarime, jana Desemba 30, 2020.

Ukarabati huo unafanyika kutokana na Sh milioni 968 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

 

“Ninawapongeza kwa kazi nzuri iliyofanyika, ukarabati huu ni jitihada zinazofanywa na Rais John Pombe Magufuli katika kuboresha shule kongwe nchini.

 

“Shule imebadilika, imekuwa nzuri, kazi imefanyika vizuri, ubora wa kazi iliyofanyika unalingana na thamani ya fedha iliyotumika. Kamilisheni kazi iliyoobaki na tunzeni miundombinu iliyokarabatiwa,” amesema Nyamhanga.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga (wa pili kulia), akiendelea kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Tarime, jana Desemba 30, 2020. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Machota Edward Kora.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tarime, Machota Edward Kora (aliyesimama) ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi shuleni hapo, akisoma taarifa ya ukarabati wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo - kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga (wa kwanza kulia waliokaa).

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu huyo wa TAMISEMI ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa juhudi zilizowezesha kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi - licha ya shule kukabiliwa na upungufu wa walimu.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Tarime, Machota Edward Kora, akizungumza na Mara Online News shuleni hapo baada ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga kukagua na kueleza kuridhishwa na maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo, jana Desemba 30, 2020.

Aidha, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Nyamhanga, ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa halmashauri nyingine nchini kuiga mfano wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa matumizi mazuri ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Sehemu ya ndani ya bweni la wanafunzi linaloendelea kukarabatiwa katika Shule ya Sekondari ya Tarime.
 

Nyamhanga ameonya kuwa ofisi yake haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya halmashauri zitakazotumia vibaya fedha za serikali zinazotengwa kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo ya wananchi.

 

“Hatua kali zitachukuliwa kwa halmashauri ambazo zitafuja fedha zinazotolewa na serikali. Hatutakuwa na uvumilivu wowote kwa matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi,” amesisitiza.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kutoa mamilioni hayo ya fedha kwa ajili ya kugharimia uboreshaji wa miundombinu ya shule hiyo ya wavulana.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa (aliyesimama), akimweleza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Joseph Nyamhanga (wa kwanza kulia waliokaa), jinsi ofisi yake inavyosaidia usimamizi wa ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Tarime.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa akionesha baadhi ya majengo ya mabweni ya wanafunzi yaliyokarabatiwa katika Shule ya Sekondari ya Tarime.

Naye Mkuu wa Shule ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi shuleni, Mwalimu Machota Edward Kora, amemshukuru Rais Magufuli akisema fedha alizotoa zimefanya maboresho makubwa ya miundombini mbalimbali ya shule hiyo, hali ambayo imewaongezea walimu hamasa ya kufundisha na wanafunzi kusoma kwa bidii zaidi.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages