NEWS

Sunday 27 December 2020

Wanamara wakutana, RC Malima asema Mara ya sasa ni neema tupu

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (aliyesimama mbele) akihutubia kongamano la Wanamara mjini Musoma, jana.

WAZALIWA wa mkoa wa Mara wanaoishi nje na ndani ya mkoa huo wakiwemo wawekezaji wazawa, jana Desemba 26, 2020 wamekutana kujadili namna ya kushirikiana katika kuufanya kuwa sehemu bora ya kuishi na kuwekeza.

 

Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Adam Malima ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt John Pombe Magufuli imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa wazawa mkoani humo.

 

“Hakuna wakati mzuri wa kuwa raia wa Mara kama kipindi cha Mheshiiwa Rais Dkt John Pombe Magufuli,” Malima amewaambia washiriki wa kongamano hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (aliyesimama) akiendelea kuhutubia kongamano la Wanamara mjini Musoma.
 

Ametoa mfano wa uwekezaji mkubwa unaotekelezwa na serikali katika sekta ya usafirshaji ukiwemo uborosheaji na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma ambao amesema utatengeneza fursa lukiki za kiuchumi mkoani.

 

“Mheshimiwa Rais ametuahidi kuwa uboreshaji na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma utatekelezwa,” amesema Malima.

Mojawapo ya ndege za Shirika la Ndege Tanzania.
 

Malima amesema mbali na mkoa wa Mara kuwa na hifadhi bora Afrika [akimaanisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti] na inayotembelewa zaidi na watu kutoka mataifa mbalimbali duniani, una fursa nyingi katika sekta za uvuvi, madini na kilimo.

Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Barani Afrika kwa miaka miwili mfululizo, yaani 2019 na 2020.

“Sisi Mara ndio tuna surface (eneo) kubwa ya Ziwa Victoria, na kahawa bora aina ya Arabica inapatikana Mara, inalimwa wilayani Tarime,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Sehemu ya washiriki wakifuatilia mada katika kongamano hilo la Wanamara.

Aidha, Malima amesema juhudu za kuutangaza mkoa wa Mara vizuri zimeendelea kuzaa matunda na hivyo kuondoa dhana potofu kuwa mkoa huo ni sehemu ya watu wakorofi na matukio mabaya.

 

Ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kuacha kubaguana, badala yake wajenge umoja na kushirikiana katika kuchapa kazi kwa kutumia rasilimali walizojaaliwa na Mungu kujiletea maendeleo.

 

“Kaulimbiu yetu iwe ni Mara yetu, Mara moja, Fahari yetu,” amesema RC Malima na kutumia nafasi hiyo pia kuwataka waratibu wa kongamano hilo ambao ni Chama cha Wafanyabishara, wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mara kuwashirikisha wabunge wa mkoa huo akisema ni wadau wakubwa wa maendeleo.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo la Wanamara wakisoma nakala ya gazeti la Sauti ya Mara linalotoka kila Jumatatu. Gazeti hilo na blogu hii ya Mara Online News vinatoa kipaumbele katika habari za uhifadhi na maendeleo.
 

Kwa upande wake, Mshauri wa Jukwa la Wanamara (Mara Forum) wanaoishi nje ya mkoa huo, Japhet Makongo, amesema wazo la kuwa na jukwaa hilo linalenga kuhamasisha wazaliwa wa Mara, hususan vijana kushiriki katika ujenzi wa Mara mpya.

 

Makongo amesema lengo jingine ni kuweka nguvu ya pamoja katika kutangaza mambo mazuri ya mkoa huo yanayohamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mkoa wa Mara pia umejaaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba inayostawisha mazao mbalimbali ikiwemo kahawa aina ya Arabica.

“Pia tumejipanga kusaidia kwenye elimu katika eneo la ufundishaji wa lugha za Kiswahili na Kiingezea. Tunatambua serikali inafanya kazi kubwa lakini tutaongeza nguvu,” amesisitiza Makongo.

 

Viongozi wengine walioshiriki kongamano hilo ni pamoja na wakuu wa wilaya, weneyeviti na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (kulia mbele) akiandika mambo muhimu yaliyowasilishwa na kujadiliwa kwenye kongamano hilo la Wanamara. Wanaomfuatia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu.

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages