NEWS

Saturday 19 December 2020

Mto Mara unavyoitangaza Tanzania kimataifa

Makundi ya nyumbu yakivuka Mto Mara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, Tanzania.
 

UKIWA katika Chuo cha Kimataifa cha Maji, IHE Delft, kilichopo chini ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) katika mji wa Delt nchini Uholanzi, hautakosa kusikia Mto Mara ukitajwa kama moja ya mito maarufu na ya kipekee kimataifa.

 

Wanasayansi waliobobea katika sekta ya maji na hifadhi wa mazingira wanauelezea Mto Mara katika chuo hicho kama mto muhimu unaostahili kutunzwa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Sehemu nyingine ya makundi ya nyumbu yakivuka Mto Mara.

 

Aidha, wanasayansi kutoka chuo hicho wamefanya tafiti mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi ndani ya ikolojia ya Mara - zinazolenga kuweka mikakati ya kuwa na uhifadhi endelevu wa mto huo na bonde lake.

 

Mto Mara ni sehemu muhimu ya ikolojia ya Serengeti na una mchango mkubwa katika uhifadhi wa wanyamapori ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imetunukiwa Tuzo ya Hifadhi Bora zaidi barani Afrika kwa miaka miwili mfululizo (2019 NA 2020).

Hivi ndivyo nyumbu wanavyoruka kuvuka Mto Mara.

 

“Mto Mara unasifika kimataifa kwanza kwa sababu unawezesha maisha ya wanyamapori katika hifadhi ya Serengeti ambayo ni kivutio cha utalii cha kimataifa,” anasema Mkurugenzi wa Shirika la Wakulima na Wavuvi (VIFAFIO) Kanda ya Ziwa, Majura Maingu.

 

Anaongeza “Pili, Mto Mara unachangia maji mengi ndani ya Ziwa Victoria ambalo pia lina uhusiano wa karibu na Mto Nile.” 

 

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) inafanya kila linalowezekana kutunza na kuhifadhi Mto Mara kupitia ofisi yake ya Dakio la Mara-Mori lililopo Musoma, huku wadau mbambali zikiwemo jumuiya za watumia maji zikishirikishwa katika jukumu hilo.

Pundamilia wakivuka Mto Mara.


“Mto Mara ni muhimu sana kwa taifa letu, nyumbu ambao ni kuvutio kikubwa cha watalii katika Hifadhi ya Serengeti wanavuka Mto Mara,” anasema Afisa Uhusiano wa LVBWB, Mhandisi Gerald Itimbula.

 

Kila mwaka watalii wamekuwa wakimiminika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea   tukio la nyumbu kuvuka Mto Mara kwenda Hifadhi ya Maasai - Mara nchini Kenya na kurudi Serengeti.

 

Mbali na uhifadhi wa wa ikolojia ya Serengeti - Mara, Bonde la Mto Mara lina mchango mkubwa katika ustawi wa maisha ya watu zaidi ya milioni 1.1 katika nchi za Tanzania na Kenya.

Mwonekano wa sehemu ya Mto Mara.

 

Mto huo ambao unaanzia kwenye chemichemi za Enopuyapui katika misitu ya Mau nchini Kenya huchangia pia kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Kenya kupitia maadhimisho ya Siku ya Mara.

 

Maadhimisho hayo hufanyika Septemba 15 kila mwaka katika kipindi cha msimu wa nyumbu kuvuka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tanzania kwenda Hifadhi ya Maasai - Mara, Kenya na kurudi Serengeti.

Mwonekano wa sehemu nyingine ya Mto Mara upande wa Tanzania.

 

Maadhimisho haya huendeshwa kwa pamoja na nchi hizi mbili za Tanzania na Kenya chini ya uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) yenye makao yake Kisumu, Kenya.

 

Mto Mara una urefu wa kilomita za mraba 13,504, kati ya hizo, asilimia 65 ziko Kenya na asilimia 35 ziko upande wa Tanzania.

 

(Imeandikwa na Mugini Jacob)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages