NEWS

Friday 8 January 2021

ATFGM Masanga yaendelea kuwezesha mafunzo mbadala ya tohara kwa watoto wa kike Tarime

Baadhi ya wasichana wa kisasa waliohitimu mafunzo mbadala ya tohara katika kituo cha ATFGM Masanga wakiimba na kucheza wakati wa mahafali yao, jana Januari 7, 2021.

WASICHANA 473 wamepata mafunzo mbadala ya tohara katika kambi okozi ya Shirika lisilo la Serikali la ATFGM Masanga lililopo wilaya ya Tarime mkoani Mara.

 

Mahafali ya 12 ya wahitimu hao yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Masanga, jana Januari 7, 2021.

Mkurugenzi wa Shirika la ATFGM Masanga, Sista Stella Mgaya akizungumza katika mahafali hayo.


Hadi sasa shirika hilo limeokoa wasichana zaidi ya 3,000 waliokuwa katika hatari ya kukeketwa.

 

Katika taarifa yake, Meneja Mradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani amesema shirika hilo pia limeshasaidia watoto 546 kupata elimu ya msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na chuo kikuu.

 

Mgani ametaja baadhi ya wadau wanaoshirikiana na ATFGM Masanga kusaidia wasichana hao kufikia ndoto zao kielumu kuwa ni Shirika la Terre des Hommes la Uholanzi, Daughters of Charity, Kindermissionswerk na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

Meneja Mradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani (kulia), akisoma taarifa ya utoaji wa mafunzo mbadala ya tohara, wakati wa mahafali hayo.

Wasichana waliopata mafunzo mwaka huu wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria wazazi, walezi, ng’ariba na wazee wa mila wanaolazimisha ukeketaji kwa watoto wa kike.

 

Pia wameiomba serikali kukomesha tabia ya wazazi na walezi wanaokataa kuwapokea watoto wao baada ya kuhitimu mafunzo mbadala ya tohara katika kituo hicho cha ATFGM Masanga.

 

Wamesema kwa kufanya hivyo, watoto hao watakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kufikia ndoto zao kielimu na kupata huduma za msingi bila kubaguliwa.

Wahitimu wa mafunzo mbadala ya tohara wakisoma risala yao wakati wa mahafali yao.

“Tunatoa shukurani nyingi kwa ATFGM Masanga kwani mbali na kuendeleza wenzetu wengi kielimu katika ngazi mbalimbali, wanatupatia elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na haki za mtoto,” amesema Lilian Chacha na kuungwa mkono na mwenzake, Grace Francis.


Huku akionekana mwenye furaha, Lilian ameongeza “Sasa mimi ni binti wa kisasa, nashukuru sana ATFGM Masanga.”

 

Kwa upande wake, Lidya Chacha aliyepata mafunzo mbadala ya tohara yanayotolewa na ATFGM Masanga tangu mwaka 2008, amesema ni miongoni mwa mabalozi wazuri wanaotoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji katika jamii zinazoendekeza mila hiyo ya ukatili wa kijinsia.

 

“Mimi na wenzangu sasa tumesadia kufanya idadi ya wasichana wanaopata elimu ya tohara mbadala katika kituo cha ATFGM Masanga kuwa kubwa kama tunavyoona katika mahafali ya mwaka huu,” amesema Lidya.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo mbadala ya tohara wakati wa mahafadili yao.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri amewahakikishia wasichana hao usalama na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayeshiriki kuwalazimisha kukeketwa.

 

Mhandisi Msafiri amesema serikali itaunga mkono juhudi za Shirika la ATFGM Masanga kwa kulichimbia kisima cha maji ili kupunguza tatizo la uhaba wa maji linalosabibishwa na ongezeko la wasichana wanaokimbilia kituoni hapo kupata mafunzo mbadala wa ukeketaji.

 

Ametumia nafasi hiyo pia kudokeza mpango wa kujenga shule ya sekondari kwa ajili ya wasichana ambao hawajakeketwa katika eneo la Nyamwaga wilayani hapa.

 

“Tayari kuna shilingi milioni 200 ambazo zimetengwa kujenga shule ya wasichana ambao hawajakeketwa,” amesema mkuu huyo wa wilaya aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (kushoto) akimkabidhi mmoja wa wasichana hao cheti cha kuhitimu mafunzo mbadala ya tohara katika kituo cha ATFGM Masanga.

Aidha, Msafiri amelipongeza Shirika la ATFGM Masanga kwa kuendelea kusaidia mamia ya wasichana ambao wamekuwa katika mazingira hatari ya kukeketwa.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages