NEWS

Saturday 9 January 2021

Mbunge Waitara akagua na kuchangia ujenzi vyumba vya madarasa Tarime Vijijini

Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amekagua na kuchangia Sh milioni tano ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Shule ya Sekondari mpya ya Kewamamba katani kiore, jana Januari 8, 2021.

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, jana Januari 8, 2021 amefanya ziara ya kukagua na kuchangia gharama za ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari jimboni humo.

 

Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), ameanza kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Regicheri ambapo amechangia Sh milioni tano kutoka Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo hilo.

Mbunge Waitara (wa pili kulia) akiwa katika Shule ya Sekondari ya Regicheri alikokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa. Kulia ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Hamis Kura na kushoto mwenye rasta ni Diwani wa Kata ya Regicheri, John Bosco.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Regicheri, Mariam Sabai, wananchi wamechangia Sh milioni 21 na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imetoa Sh milioni 20 kuchangia gharama za ujenzi huo kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kupata nafasi ya kusomea.

 

Baada ya hapo Mbunge Waitara amezuru katika Shule ya Sekondari mpya ya Kewamamba ambapo ametoa Sh milioni saba kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na kuwapongeza wananchi kwa juhudi kubwa wanazoelekeza kwenye ujezi huo.

 

Diwani wa Kata ya Kiore, Rhobi John amesema kujengwa kwa shule hiyo kutakuwa msaada kwa wanafunzi waliokuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kusoma Shule ya Sekondari ya Nkerege.

Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara akishiriki kwa vitendo katika ujenzi wa miundombinu ya Shule ya Sekondari mpya ya Kewamamba katani Kiore.

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Hamis Kura aliyefuatana na Mbunge Waitara katika ziara hiyo amewapongeza wananchi wa kata Kiore kwa kushirikiana katika kujenga vyumba vitano vya madarasa ya Shule ya Sekondari mpya ya Kewamamba.

 

Akiwa katani Komaswa, Mbunge Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Manga linalogharimu Sh milioni 100 ambazo ni fedha za EP4R.

Mbunge Waitara katika Shule ya Sekondari ya Manga alikokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na bwalo la chakula.

Baadaye Mbunge Waitara amekwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Bukenye katika kijiji cha Bisarwi katani Manga, ambapo amechangia Sh milioni 10 kuchangia ujenzi wa vyoo.

 

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Manga, Noel Chacha amesema wananchi wamejenga vyumba vinne vya madarasa kwa gharama ya Sh milioni 38, kati ya hizo, Sh milioni 19 ni michango ya wananchi.

Mbunge Waitara (kushoto) akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Bukenye katani Manga.

“Shule zote mpya zilizojengwa kwa juhudi za wananchi zitafunguliwa mapema mwaka huu kabla ya mwezi wa pili [Februari] na watoto watasoma,” amesema Waitara.

 

Pia Mbunge Waitara amekagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba saba vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nkerege katani Kiore na kuwapongeza wananchi kwa kujenga vyumba vitano kwa michango yao wenyewe huku vyumba viwili vya madarasa vikijengwa na Halmashauri.

 

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkerege, Mwita Mwise amemshukuru Mbunge Waitara kwa jitihada zake zilizofanikisha kufunguliwa kwa shule hiyo na wanafunzi kuanza masomo mwaka 2020.

Mbunge Waitara (kulia) akikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Nkerege. Wa pili kulia aliyenyoosha mkono ni Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Kura.

Wakati huo huo, wananchi wa kijiji cha Nyagiswa wamemwomba Mbunge Waitara akakubali kwenda kuona eneo wanakoanza ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho na kuchangia ujenzi huo Sh milioni tano.

Mbunge Waitara (wa pili kushoto mbele) akifuatana na wakazi wa kijiji cha Nyagiswa kwenda kuona aneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Wa kwanza kushoto ni Katimu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Marema Sollo. 

(Habari na Picha zote na Geofrey John wa Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages