NEWS

Friday 8 January 2021

Waziri Aweso ammiminia sifa Mkurugenzi wa MUWASA

Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru akisoma taarifa ya utendaji wa Mamlaka hiyo kwa Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (hayupo pichani) mjini Musoma, jana Januari 7, 2021.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA), CPA Joyce Msiru kutokana na utendaji wake mzuri unaoiwezesha Mamlaka hiyo kutoa huduma bora ya maji kwa wananchi.

 

“Hongera sana madam [CPA Joyce Msiru], ulifanya kazsi nzuri Moshi na unafanya kazi nzuri sana hapa [Musoma],” Waziri Aweso amemwambia Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MUWASA katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya kukagua miradi ya maji mkoani Mara, kilichofanyika mjini Musoma, jana Januari 7, 2021.

Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso (aliyesimama) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru (wa kwanza kushoto), kutokana na utendaji kazi wake mzuri katika Mamlaka hiyo.

Aweso amesema Wizara ya Maji itaendelea kutoa fedha kupitia MUWASA kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji inayosimamiliwa na Mamlaka hiyo ili ikamilike kwa wakati.

 

“Sisi kama Wizara hatutakuwa kikwazo kwa Mamlaka hii [MUWASA), mkihitaji pesa sema tutawa- support (tutwapatia),” amesema Waziri huyo.

 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima ameeleza kuridhishwa na utendaji kazi wa Mamlaka hiyo. “MUWASA sasa wanafanya vizuri,” amesema Malima.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Kighoma Malima akizungumza katika kikao hicho. Kushoto ni Waziri wa Maji, Jumaa Hamidu Aweso.

CPA Msiru ameweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza MUWASA tangu kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo.

 

Mkurugenzi Mtendaji huyo amemweleza Waziri Aweso kuwa hadi sasa MUWASA imefanikiwa kufikia asilimia 95 ya wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma wanaopata huduma ya maji ya bomba.

 

Mafanikio mengine ambayo MUWASA imeyapata katika kipindi kifupi cha uongozi wa CPA Msiru ni kuwafungia wateja wote wa Mamlaka hiyo mita.

 

Katika taarifa yake, CPA Msiru amesema serikali imetumia Sh bilioni 47 kuboresha huduma ya maji katika Manispaa ya Musoma ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.

 

Ufungaji huo wa mita umesadia kupunguza kiwango cha upotevu wa maji (non-revenue for water).

Maofisa wa idara mbalimbali za serikali mkoani Mara wakishiriki kikao hicho.

Kitaaluma, CPA Msiru ni Mhasibu, lakini ameamua kujikita katika utumishi huo wa umma kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora ya maji safi na salama ya bomba.

 

Hata hivyo, CPA Msiru ametaja baadhi ya vikwazo vinavyoikabili MUWASA kuwa ni deni la Sh biloni 1.1 ambazo inazidai taasisi mbalimbali za umma, wizi wa maji na uharibifu wa miundombinu ya maji unaofanywa na baadhi ya watu, hasa nyakati za usiku.

 

Kuhusu wizi wa maji, Waziri Aweso amemtaka Mkurugenzi Mtendaji huyo MUWASA kutokuwa na huruma kwa wezi wa maji.

 

“Wezi shughulika nao, chukua hatua kwa wale wote ambao ni wezi wa maji,” amesema Waziri Aweso.

 

Hivi karibuni CPA Msiru ametaja maeneo ambayo yamekuwa sugu katika kuchomoa mabomba na kukinga maji kwa wizi, hasa nyakati za usiku kuwa ni Kigera, Nyakato, Makoko, Nyamatare, Buhare na Mwisenge.

 

Ametoa onyo kwa wanaofanya vitendo hivyo vya uhalifu kuacha mara moja na kufuata utaratibu wa kupata huduma ya maji.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages