NEWS

Sunday 10 January 2021

Kushtakiwa kwa Trump: Democrats wajiandaa kuchukua hatua dhidi ya ghasia za Capitol Hill

Mbunge wa South Carolina James Clyburn, katika picha na spika wa bunge la uwakilishi Nancy Pelosi wamekuwa wanandani wa Joe Biden
Bunge La wawakilishi nchini Marekani huenda likapiga kura mapema siku ya Jumanne kuhusu kifungu cha sheria cha kumshtaki rais Donald Trump, afisa mkuu wa chama hicho amesema.

Wabunge wa Democrats wanapanga kumshtaki bungeni Rais Trump kwa 'malipo ya uasi' dhidi ya hatua yake ya 'kuchochochea ghasia' zilizosababisha uvamizi wa jumba la Bunge la Capitol Hill.

Kiranja wa bunge James Clyburn aliambia CNN kwamba hatua zitachukuliwa wiki hii. Lakini chama hicho huenda kisitumie kifungu chochote cha sheria katika bunge la seneti ili kumfungulia mashtaka hayo hadi rais mteule Joe Biden atakapohudumu siku zake 100 za kwanza ofisini.

''Tumpatie rais Mteule Joe Biden siku 100 za kwanza ili aanzishe ajenda yake ya utawala'', alisema bwana Clyburn.

Hatua hiyo itamruhusu bwana Biden kuthibitisha baraza lake jipya la mawaziri na kuanzisha sera muhimu ikiwemo kukabiliana na virusi vya corona kitu ambacho kitalazimika kusubiri iwapo bunge la seneti litakuwa limepokea vifungu hivyo vya kumshtaki rais Donald Trump.

Bwana Trump hajatoa taarifa yoyote kwa umma tangu alipofungiwa na baadhi ya mitandao ya kijamii ikiwemo Twitter siku ya Ijumaa.

Siku ya Jumapili hatahivyo , Ikulu ya Whitehouse ilitangaza kwamba rais huyo ataelekea katika jimbo la Texas siku ya Jumanne ili kutembelea eneo la ukuta wa mpakani na Mexico ili kuangazia kazi ya utawala wake eneo hilo.

Bwana Trump ameshutumiwa na wanachama wa Democrats na idadi ndogo ya wanachama wa Republican kwa kuchochea ghasia za Jumatano iliopita ambapo takriban watu watano walifariki.

Lakini hakuna hata mwanachama mmoja wa Republican amesema kwamba atapiga kura ya imani dhidi yake kwa makosa hayo katika seneti.

Seneta wa pili wa chama cha Republican Pat Toomey alimtaka rais Trump kujiuzulu siku ya Jumapili.

''Nadhani njia bora kwa taifa letu ...ni kwa rais kujiuzulu na kuondoka haraka iwezekanavyo'', alisema Seneta Toomey akizungumza na chombo cha habari cha NBC.

'' Natambua kwamba hilo huenda lisifanyike lakini nadhani ndio njia bora''

Lisa Murkowski, kutoka jimbo la Alaska, alikuwa seneta wa kwanza wa Republican kumwambia rais kuondoka mmamlakani .

Ben Sasse , seneta wa Republican kutoka Nebraska amesema kwamba atafikiria kuhusu kupiga kura dhidi ya vifungu hivyo iwapo vitapitishwa na bunge hilo.

Wakati huohuo aliyekuwa seneta wa California Arnold Schwarzenegger alimtaja rais Trump kuwa rais mbaya zaidi katika video moja ya mtandaoni.

Muigizaji huyo alifananisha ghasia za siku ya Jumatano na zile za Kristallnacht, au usiku wa glasi zilizovunjwa ambapo mali ya Wayahudi iliharibiwa na watu wa Nazi kutoka Ujerumani 1938.

Huku wachunguzi wakijaribu kuwashtaki waandamanaji waliovamia bunge , idara za polisi huko Virginia na Washington ziliwapatia likizo maafisa wa polisi waliolazimika kurudi kazini wakati walipokuwa likizo.

Idara za zima moto mjini Florida na New York pia zimesema kwamba baadhi ya wanachama wake huenda walikuwepo wakati waandamanaji wapolivamia jumba la capitol Hill kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Ikulu ya Whitehouse imepuuzilia mbali kura hiyo ya maoni kama inayochochowa kisiasa hatua ambayo huenda ikazidisha mgawanyiko unaoshuhudiwa nchini humo.

Iwapo mpango huo utaendelea , bwana Trump huenda akawa rais wa kwanza katika historia ya Marekani kushtakiwa na bunge mara mbili.

''Kwa hilo kufanyika , mashtaka dhidi yake ni sharti yawasilishwe bungeni na kupitishwa kwa kura. Huenda ikawa siku ya Jumanne au Jumatano kabla hatua kuchukuliwa, alisema kiranja wa bunge Bwana Clyburn akiambia CNN, lakini nadhani itafanywa wiki hii''.

Baadaye kura hiyo itawasilishwa katika bunge la seneti ambapo thuluthi mbili ya kura itahitajika kwa rais kuondolewa madaraka

Iwapo atapatikana na hatia bunge la seneti pia huenda likapiga kura ya kumzuia Rais Trump kushikilia nafasi yoyote serikalini.

Hatahivyo bwana Clyburn , mbunge wa bunge la wawakilishi kutoka South Carolina alisema kwamba hadhani itakuwa rahisi kumshtaki Rais Trump na kupiga kura ya kutokuwa na imani naye kabla ya rais Trump kuondoka ofisini siku 10 zijazo.

Badala yake , Democrats wanafikiria kuchelewesha kuwasilisha vifungu vya kura ya kutokuwa na imani naye katika bunge la seneti.

Tayari wamemtaka makamu wa rais Mike Pence kutumia kifungu cha sheria kitakachomruhusu kuwa kaimu rais Siku ya Jumapili.

Spika wa bunge la uwakilishi Nancy Pelosi alisema kwamba wabunge wiki hii watapiga kura kuhusu maamuzi ya kumtaka makamu wa rais Mike Pence kumuondoa madarakani bwana Trump mara moja kabla ya kushtakiwa bungeni.

Hatahivyo , ijapokuwa bwana Pence ameonekana kujiepusha na rais huyo kwa kusema siku ya Jumapili kwamba anapanga kuhudhuria kutawazwa kwa ais mteule Joe Biden tarehe 20 mwezi Januari , hakuna ishara kwamba makamu huyo wa rais atatumia kufungu hicho cha sheria.

Bwana Trump amesema kwamba hatohudhuria sherehe ya kutawazwa kwa Joe.

Sasa amekiri kushindwa katika uchaguzi wa urais wa Novemba 3 na ameahidi kuachia madaraka kwa njia ya amani licha ya kuendelea kutoa matamshi yasio na ushahidi kuhusu wizi wa kura.

Bwana Joe Biden amesema kwamba kura hiyo ya kutokuwa na imani ni ya bunge kuamua lakini alikuwa ameshikilia kauli ya kwamba rais Trump hakuwa na uwezo wa kuongoza taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages