Mtandao wa kijamii wa Twitter umeifunga moja kwa moja akaunti ya rais Donald Trump, ukielezea kitisho cha uchochezi zaidi wa vurugu, kufuatia uvamizi uliofanywa na wafuasi wake katika majengo ya bunge siku ya Jumatano.
Twitter imetangaza kuifunga moja kwa moja akaunti binafsi ya rais Trump na ile ya kampeni ya kiongozi huyo kufuatia vurugu za bungeni katikati mwa wiki hii. Kwenye taarifa yake, Twitter imesema baada ya kupitia jumbe za hivi karibuni za akaunti binafsi na maudhui yake, imeamua kuifungia moja kwa moja kwa sababu ya kitisho cha uchochezi zaidi.
"Kwa muktadha wa matukio ya kutisha ya wiki hii, tuliweka wazi siku ya Jumatano kwamba ukiukwaji zaidi wa sheria za Twitter utasababisha uwezekano wa hatua kama hizi", ilisema kampuni ya Twitter katika taarifa yake
Trump asema Twitter inabinya uhuru wa kujieleza
Rais Donald Trump |
Trump alijaribu kuzima jaribio la kumfungia usiku wa Ijumaa kwa kuandika kupitia akaunti rasmi ya rais wa serikali ya Marekani akisema "wanajaribu kuninyamazisha".
Ujumbe wake uliendelea kusema kwamba "Twitter imekwenda mbali zaidi kubinya uhuru wa kujieleza na usiku huu wafanyakazi wa Twitter wameshirikiana na Democrats kuondoa akaunti yangu kwenye majukwaa yao, kuninyamazisha na nyinyi wazalendo milioni 75 mlionipigia kura", ulisomeka ujumbe wa Trump kupitia ukurasa wa serikali ya Marekani.
Hata hivyo Ujumbe huo ulifutwa kutokana na kwamba Twitter hairuhusu matumizi ya akaunti nyingine ili kukwepa kusimamishwa. Uamuzi huo wa Twitter ulikuja saa chache baada ya Trump kurejeshewa akaunti yake baada ya kusimamishwa kwa muda siku ya alhamis. Kufungwa moja kwa moja kwa akaunti hiyo kunamzuia rais Trump kutumia moja ya njia zake kuu ya kuwasiliana na umma na kuelezea sera pamoja na kauli binafsi.
Kwa mujibu wa Twitter, Trump aliandika yafuatayo siku ya Ijumaa;
Akaunti ya Trump iliyosimamishwa |
"Wazalendo milioni 75 walionipigia kura, Marekani kwanza na kuifanya Marekani kuwa bora tena, watakuwa na sauti kubwa katika siku za usoni. Hawatodharauliwa au kutotendewa haki kwa njia yoyote".
Ujumbe huo ulifuatiwa na ujumbe mwingine, ambapo Trump alitangaza kwamba hatohudhuria kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden. "Kwa wengi mlioniuliza, sitohudhuria siku ya kuapishwa Januari 20".
Twitter imesema inaisimamisha akaunti ya Trump iliyo na wafuasi zaidi ya milioni 88, juu ya ukiukwaji wa sera zake dhidi ya kuhimiza vurugu.
Facebook nayo yachukua mkondo huo
Trump pia amezuiliwa kwa muda usiojulikana katika ukurasa wa Facebook na kampuni yake tanzu ya Instagram, huku shinikizo likizidi kwa mitandao hiyo mikubwa kufuta moja kwa moja akaunti za rais huyo.
Wito huo unafuatia kuvamiwa kwa majengo ya bunge siku ya Jumatano, ambako kulishuhudia wafuasi wanaomuunga mkono Trump wakivuruga kikao cha pamoja cha bunge huko Washington DC ili kuthibitisha ushindi wa Rais mteule Joe Biden katika uchaguzi wa 2020.
No comments:
Post a Comment