NEWS

Tuesday 19 January 2021

Mkurugenzi Apoo ajivunia mafunzo ya madiwani Tarime Vijijini

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Apoo Castro Tindwa.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Apoo Castro Tindwa amesema mafunzo ya kuwajengea uwezo madiwani wa halmashauri hiyo yataongeza uhusiano na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kuwatumikia wananchi.

 

Tindwa ameyasema hayo katika mahojiano na Mara Online News baada ya ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku mbili - yaliyoanza leo Januari 19, 2021 katika mji mdogo wa Nyamwaga.

 

“Uhusiano utaongezeka kati ya madiwani na watumishi, lakini pia ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za halmashauri utaongezeka, maana kila mtu sasa atakuwa anajua mipaka yake ya kazi.

 

“Umoja ni nguvu, tufanye kazi kwa pamoja na ninawahimiza watumishi wenzangu tuwape ushirikiano wa kutosha hawa wenzetu [madiwani] ili tuipaishe halmashauri yetu kimaendeleo,” amesema Tindwa.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) wakiwa katika mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wa kusimamia uendeshaji wa halmashauri.

Mafunzo hayo yamegharimiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) kwa lengo la kuwajengea madiwani hao uwezo wa kusimamia uwendeshaji wa halmashauri hiyo.

 

Baadhi ya mada za mafunzo hayo zilizowasilishwa na wataalamu ni kuhusu sheria za uendeshaji wa mamlaka za serikali za mitaa, utawala bora na ushirikishaji wananchi, muundo, madaraka na majukumu ya serikali za mitaa.

 

Mada nyingine ni kuhusu uendeshaji wa vikao na mikutano katika mamlaka za serikali za mitaa, uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi shirikishi katika jamii, usimamizi na uthibiti wa fedha katika mamlaka ya serikali za mitaa.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages