NEWS

Wednesday 17 March 2021

Buriani Rais Magufuli

Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, wakati wa uhai wake.
 

RAIS wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli ameaga dunia Jumatano Machi 17, 2021 saa 12 jioni jijini Dar es Salaam - akiwa na umri wa miaka 61.

 

Kifo cha Rais Magufuli kimetangazwa na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, kwamba amefariki dunia akiwa katika Hospitali ya Mzena alikokuwa anapata matibabu ya maradhi ya moyo.

 

Katika hotuba yake kwa umma, Samia amefafanua kuwa Rais Magufuli alianza kuugua na kulazwa hospitalini hapo Machi 14, 2021. Kabla ya hapo alikwenda kupata matibabu Machi 6 na kuruhusiwa Machi 7, 2021.

Pumzika kwa amani Rais Dkt John Pombe Magufuli - mtetezi wa wanyonge.
 

Mkuu huyo wa nchi amefariki akiwa chini ya uangalizi wa madaktari wa moyo kutoka Hospitali ya Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Samia.

 

Kutokana na msiba huo mkubwa, Makamu wa Rais ametangaza siku 14 za maombolezo huku bendera zote nchini zikipepea nusu mlingoti.

 

Kulingana na Katiba ya Tanzania, Makamu wa Rais atashika hatamu ya kuongoza nchi kwa muda uliosalia kukamilisha miaka mitano ya mhula wa pili unaoishia mwaka 2025.

 

Tayari viongozi kutoka mataifa mbalimbali wameanza kutuma risala za rambirambi kwa Watanzania na familia ya Magufuli. Viongozi hao ni pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Mwinyi na Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya.

 

Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani Rais Dkt John Magufuli na kutujaalia amani na uvumilivu, amina.

 

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages