NEWS

Saturday 24 April 2021

Kwanini wana-Shirati hawatamsahau Waziri Aweso

Kutoka kushoto ni Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga wakati waziri huyo alipofanya ziara ya kukagua miradi ya maji wilayani humo, hivi karibuni.
 

WAKAZI wa mji mdogo wa Shirati katika wilaya ya Rorya mkoani Mara wameishukuru Serikali kwa kuwarejeshea huduma ya maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria baada ya kuikosa kwa miaka sita kutokana na ubovu wa miundombinu husika.

 

Huduma hiyo imerejeshwa na Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) iliyoagizwa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kukarabati miundombinu ya mradi wa maji iliyokuwa imeharibika na hivyo kuwakosesha wakazi wa mji huo maji ya bomba tangu mwaka 2015.

Mkazi wa mjiwa Shirati akishuhudia usafi wa maji ya bomba katika kimojawapo cha vituo vya maji, huduma ambayo imereshwa hivi karibuni baada ya kukosekana kwa miaka sita.
 

Januari 6, 2021, Waziri Aweso alifanya ziara katika mji wa Shirati wenye wakazi 30,804 ambapo katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliiagiza MUWASA kukarabati miundombinu ya mradi huo ili kurejesha huduma ya maji ya bomba kwa wakazi wa mji huo.

 

Siku hiyo hiyo, Waziri Aweso aliahidi kuipatia MUWASA Sh milioni 247 kwa ajili ya kugharimia ukarabati wa miundombinu hiyo, ahadi ambayo ilitekelezwa Januari 27, mwaka huu.

 

Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima aliyekwenda kukagua urejeshaji wa huduma ya maji ya bomba katika mji wa Shirati wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru amesema ukarabati wa miundombinu ya mradi huo ulianza baada ya ofisi yake kupokea fedha hizo.

Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga, Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru na wakazi wa Shirati wakishuhudia shehemu ya mabomba ya maji yaliyokarabatiwa na kuwezesha urejeshaji wa huduma hiyo katika mji huo, wiki iliyopita.
 

“MUWASA imetekeleza kwa asilimia 100 awamu ya kwanza (mpango wa muda mfupi) ya ukarabati wa miundombinu ya maji katika mji wa Shirati - uliohusisha kazi mbalimbali,” amesema CPA Msiru. 

 

Msiru ametaja kazi hizo kuwa ni marekebisho ya mashine ya kusukuma maji katika kituo cha Michire (yenye uwezo wa kusukuma maji kwa mita za ujazo 21 kwa saa) na nyingine yenye uwezo wa kusukuma maji kwa mita za ujazo 90 kwa saa - kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika mji wa Shirati, hususan katika kipindi cha mpito kuelekea ununuzi wa mashine mpya.

 

Pia, marekebisho makubwa ya mabomba ya njia kuu ya kusafirisha maji kutoka kituo cha kusukuma maji cha Michire mpaka kwenye tenki la kuyahifadhi lililopo katika kilele cha mlima Obhoke kwa urefu wa kilomita tano.

 

“Katika urefu huo, mabomba mapya yenye kipenyo cha milimita 200 yalilazwa kwa urefu wa mita 1,330. Ukarabati mwingine ni wa tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 1,500,000 lililopo eneo la mlima Obhoke na mfumo wa usambazaji maji kwa kuweka bomba mpya kwa urefu wa kilomita saba,” ameongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MUWASA.

 

Kwa mujibu wa CPA Msiru, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ya bomba kwa wakazi wa mji wa Shirati kutoka Ziwa Victoria kupitia tenki lenye ukubwa wa mita za ujazo 1,500 kwa sasa ni wateja 155 wakiwemo wa majumbani 146, taasisi nne, vioski vitatu na wafanyabiashara wawili.

 

“Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya mradi wa maji ya bomba iliyokuwa imeharibika na kutukosesha maji kwa miaka sita, sasa hivi wana-Shirati tunapata maji safi kama zamani,” amesema mkazi wa Shirati, Stela Otieno katika mazungumzo na Mara Online News.

Huduma ya maji ya bomba kama hii sasa inapatikana katika maeneo mengi ya mji wa Shirati.
 

Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Msiru amesema wamepokea maombi mengi kutoka kwa wakazi wa vijiji vya Obwere, Michire, Obhoke, Ngasaro na Kabwana wanaohitaji kuunganishiwa huduma ya maji ya bomba.

 

Hata hivyo, amesema MUWASA imewasilisha kwa Wizara ya Maji ombi la Sh milioni 366 kwa ajili ya kutekeleza mpango wa muda wa kati utakaohusisha ununuzi na ufungaji wa mashine moja ya kusukuma maji yenye uwezo mkubwa wa kusukuma mita za ujazo 90 kwa saa ili kukithi mahitaji ya maji kwa wakazi 30,804 wa mji wa Shirati na vijiji jirani.

 

CPA Msiru ametaja vijiji hivyo na idadi ya wakazi ikiwa kwenye mabano kuwa ni Laranya (3,014), Nyaera (3,036), Mabatini (2,408), Kyariko (2,876) na Nyamasyeki (2,610).

 

Ameongeza kuwa fedha hizo zitatumika pia kugharimia marekebisho ya kisima cha kuhifadhi maji kutoka Ziwa Victoria, ulazaji wa bomba kubwa lenye kipenyo cha inchi 12 la kusafirisha maji kutoka ziwani kwenda kwenye kituo cha kusukuma maji ili kuongeza wingi wa maji kulingana na ukubwa wa mashine za kusukuma maji zitakazofungwa.

 

“Matumizi mengine ya fedha hizo ni upanuzi wa mtandao wa mabomba ya kusambaza maji (umbali wa kilomita tano) kuelekea maeneo ya makazi mapya, ununuzi wa ‘bulk meter’ sita zenye kipenyo cha inchi tatu, mita za wateja 1,000 na vitendea kazi.

 

“Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha upatikanaji wa maji safi na salama na utahudumia wakazi zaidi ya 43,000 wa mitaa mitano ya mji wa Shirati na maeneo ya vijiji vya Laranya na Nyaera,” amesema Msiru.

Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya Mamlaka hiyo kwa Waziri Aweso (hayupo pichani) mjini Musoma, hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, MUWASA imepokea barua ya kukabidhiwa kwa muda uendeshaji wa mradi wa maji katika mji mdogo wa Shirati.

 

Msiru amesema baada ya ofisi yake kupokea barua hiyo, ilifanya kikao na viongozi wa mji wa Shirati wakiwemo afisa mtendaji wa mji, diwani husika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Watumia Maji Shirati na wenyeviti wa mitaa yote mitano inayounda mji huo.

 

“Kikao hiki kilisaidia kupanga mikakati ya kusambaza maji kwa wananchi. Aidha, afisa mtendaji aliipatia MUWASA vyumba vitatu vya ofisi, na tayari tumeanza kutembelea wateja wa mahitaji ya maji,” amesema CPA Msiru.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages