MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Mhandisi Robert Gabriel Luhumbi ameridhishwa na utekelezaji wa mradi ya zahanati ya kijiji cha Koreri na ujenzi wa kituo cha Polisi katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.
Mhandisi Luhumbi ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo Juni 4 na 5, 2021, alipokuwa akikagua miradi inayotarajiwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021.
“Kuna haja ya kuwaleta watu wengine kutoka mkoa huu kujifunza hapa katika utekelezaji na usimamizi wa miradi ya serikali,” amesema RC Luhumbi.
RC Luhumbi (kulia) akipitia taarifa ya utekelezaji wa miradi ya jamii wilayani Serengeti
Katika mradi wa ujenzi wa zahanati ya Koreri, mradi ulipewa Shilingi milioni 85.250 ambapo tayari umekamilika sambamba na vyoo, kichomea taka na matanki ya maji kwa gharama Shilingi milioni 75, na fedha zilizobakia zimetumika kuanza ujenzi wa nyumba ya mtumishi.
Zahanati
“Huu ni mfano mzuri sana, sehemu nyingine wanajenga zahanati kama hii kwa bei kubwa zaidi na sio kwa ubora huu na bila vitu vingine kama vyoo, kichomea taka na mfumo wa kuvuna maji ya mvua,” amesema Luhumbi.
Mradi wa ujenzi wa kituo cha Polisi katika stendi ya mji wa Mugumu, umegharimu Shilingi milioni 46, ikiwa pamoja na kuwekewa thamani zake muhimu.
RC Luhumbi pia amekagua miradi ya ujenzi wa ofisi ya Shirika la Taifa la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Serengeti, TEHAMA, barabara ya lami na mfumo wa kukusanya mapato wa GOTHOMIS katika iliyokuwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Serengeti.
RC Luhumbi ambaye amefuatana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa (KUU) wa Mara katiika ziara hiyo, amekagua pia miradi ya ujenzi wa ofisi ya kijiji, bwawa la maji, bwalo la shule na eneo la Robanda, ambapo Mwenge wa Uhuru utapokewa kutoka mkoa wa Arusha Juni 22, 2021.
Bwawa la maji
Mkoa wa Mara unatarajia kupokea Mwenge siku hiyo na kuukimbiza katika wilaya sita hadi Juni 27, 2021 na kuukabidhi katika mkoa wa Simiyu Juni 28, 2021.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2021, zimezinduliwa katika mkoa wa Kusini Unguja Mei 17, 2021 na zitafikia kilele chache Oktoba 14, 2021 katika wilaya ya Chato mkoani Geita.
(Habari na picha zote: Isyaga Mwita, Serengeti)
No comments:
Post a Comment