NEWS

Tuesday 13 July 2021

Hifadhi ya Serengeti yazindua ununuzi wa tiketi kwa watalii wa ndani Tarime
WANANCHI wamejitokeza kununua tiketi za safari maalum ya kwenda kufanya utalii wa ndani, iliyopewa jina la “kuwapokea nyumbu” katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kupitia lango la Lamai lililopo kijiji cha Karakatonga/Gibaso wilayani Tarime, Mara.

Afisa Mhifadhi Mkuu, Tutindiga George ambaye ni Mkuu wa Kitendo cha Utalii katika hifadhi hiyo, amezindua ununuzi wa tiketi hizo katika hoteli ya Goldland mjini Tarime, leo Julai 13, 2021.


Mhifadhi Tuti akikabidhi tiketi za utalii wa ndani

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Tutindiga ambaye amefuatana na Mhifadhi Mkuu, Masesa Augustine kutoka Hifadhi ya Serengeti, amesema uzinduzi huo ni wa kihistoria kwa hifadhi hiyo, eneo la Lamai na wilaya ya Tarime kwa ujumla.

Ameongeza kuwa uzinduzi huo ni mkakati wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wa kuhamasisha watalii wa ndani kutoka Tarime.


Ununuzi wa tiketi ukiendelea

“Wana-Tarime wana kila sababu ya kujivunia uzinduzi wa lango hili [Lamai], kwani ni fursa kubwa kwa wao kushiriki utalii wa ndani katika hifadhi hii [Serengeti],” amesema Mhifadhi Tuti na kuendelea:

“Tumeona tufungue lango hili [Lamai] kwa kuhamasisha utalii wa ndani kutoka wilaya ya Tarime, vikiwemo vijiji vinavyozunguka hifadhi, ili wawe mabalozi wa kwanza, wawe ma- champion wa kwenda kuonesha mkoa wa Mara kwa ujumla, kwamba Tarime sasa tumeamka, yaani ni zamu ya wana-Tarime.”

Mhifadhi huyo ametoa hamasa kwa wananchi wanaojitokeza kununua tikezi hizo kuwa mabalozi kwa kuwatangazia wengine, vikiwemo vikundi mbalimbali katika jamii kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo ya utalii wa ndani, kwa gharama nafuu.


Miongoni mwa wanunuzi wa tiketi hizo ni Rhoda Mugini (kushoto), ambaye ni mke wa CEO wa Mara Online, Jacob Mugini (mwenye koti la bluu)

“Huu ni mwanzo wa utalii wa ndani kwa wilaya ya Tarime, ambapo kwa muda hii fursa ilikuwa bado haijawezekana. Kwa hiyo watalii wa ndani kutoka Tarime wataweza kuona misafara ya nyumbu kwa ukaribu zaidi.

“Ni mwenda wa saa moja unakuwa umeshafika eneo la Lamai na kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea maajabu, ni eneo la kipekee sana ambalo watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani wanalitembelea.

“Kuanzia Julai mpaka Oktoba [kila mwaka] watalii kutoka mataifa mbalimbali wanakuja kujionea makundi ya nyumbu wanavyovuka mto Mara, ni kivutio cha kipekee, kwa kweli tunasema tuna Serengeti moja Tanzania, lakini tuna Serengeti moja duniani, hakuna sehemu nyingine unapoweza kukuta wanyama wengi wakiwa wanavuka mto, maajabu haya yanatokea Tarime upande wa Kaskazini,” amesema Mhifadhi Tuti.


Thabita (kushoto) akipokea tiketi yake kutoka kwa Mhifadhi Tuti

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inahamasisha safari ya utalii wa ndani, itakayofanyika Julai 25, 2021 kupitia lango la Lamai lililopo kijiji cha Karakatonga/Gibaso wilayani Tarime, kwa kushirikiana na taasisi ya Mara Online na kampuni ya Goldland Hotel & Tours. Kaulimbiu ya safari hiyo inasema “Wanyamapori Wetu, Utalii Wetu”.

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages