NEWS

Sunday 29 August 2021

Chama cha ushirika WAMACU chaongoza kwa kutoa bei nzuri malipo ya pili kwa wakulima wa kahawa






HATUA ya Wakulima wa Mara Cooperative Union (WAMACU) ya kununua kahawa kwa fedha taslimu (cash) na kuwalipa wakulima wa zao hilo malipo ya pili, imetajwa kuchochea hamasa ya kilimo hicho katika wilaya ya Tarime.

Hivi karibuni, WAMACU imelipa malipo ya pili kiasi cha Sh milioni 113 kwa wakulima waliouza kahawa aina ya Hard Arabica kwa chama hicho cha ushirika msimu uliopita.

“Tulikusanya kahawa kwa bei ya shilingi 1,200 kwa kila kilo moja, lakini baada ya kuuza na kupata faida, tumewalipa wakulima malipo ya pili ya shilingi 400 kwa kila kilo moja.

“Tumetoa malipo hayo ya pili kwa sababu lengo la ushirika huu ni kuinua wakulima,” Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU, Samwel Gisiboye ameiambia Mara Online News ofisini kwake, hivi karibuni.


Mkulima wa kahawa shambani

Wakizungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti wilayani Tarime hivi karibuni, wakulima wa kahawa na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS), wameishukuru WAMACU kwa kuonesha dhamira ya kuwakwamua kutoka kilimo cha kujikimu kwenda chenye tija.

Mkulima wa kahawa, John Mwera ambaye pia ni Mwenyekiti wa AMCOS ya Itiryo, anasema malipo ya pili yaliyotolewa na WAMACU yamewaongezea ari ya kukazania kilimo hicho.

“Katika pitapita yangu tangu WAMACU walipe malipo ya pili kwa wakulima waliouza kahawa msimu uliopita, nimeona mashamba yanapaliliwa na kuwekewa mbolea kwa bidii, wengi wamechangamkia kilimo cha zao hili tofauti na siku za nyuma,” Mwera anasema.

Mkulima mwingine, Mniko Mseti kutoka kijiji cha Nyantira, anasema malipo ya pili yamewezesha wakulima wengi, akiwemo yeye kuboresha mahitaji muhimu ya kifamilia na kilimo hicho.

“Haya malipo ya pili yametusaidia katika mambo mengi, baadhi tumeyatumia kuwalipia watoto wetu ada za shule, lakini pia kununua mahitaji ya shamba kama vile mbolea. Kiukweli wakulima tumefurahi sana na tumeongeza bidii mashambani,” anaeleza.


Mkulima mwingine wa kahawa shambani

Keraryo Silas kutoka kijiji cha Kangarian, anasema wakulima sasa wanaitazama WAMACU kama mkombozi wao wa kiuchumi, kwani licha ya kutoa malipo ya pili, inanunua kahawa kwa fedha taslimu.

“Utaratibu huu wa WAMACU umeleta faraja kubwa kwa wakulima, kwa sababu kwanza haikopi kahawa ya mkulima, inanunua kwa ‘cash’ na soko la zao hili sasa ni la uhakika,” Silas anasema na kuongeza:

“Kumbuka mkulima anakuwa ameshauza kahawa bila makubaliano ya kuongezewa fedha, lakini ghafla WAMACU inampatia malipo ya pili, hii ni asante kubwa. Kwa hiyo wakulima wote tunahamasishana kuuza kahawa kupitia AMCOS ili tuweze kupata malipo ya pili.”

Mwenyekiti wa WAMACU, David Hechei anasema uwepo wa chama hicho cha ushirika na utoaji wa malipo ya pili, umesaidia kupandisha bei ya kahawa na kuongeza hamasa kwa wakulima wa zao hilo la biashara.


Mwenyekiti wa WAMACU, David Hechei

Wakulima hao wanasema sasa hawana sababu ya kuuza kahawa kwa wanunuzi binafsi, kwani hawana nia ya kumkomboa mkulima, ndiyo maana hawatoi malipo ya pili kama inavyofanya WAMACU.

“Wanunuzi binafsi wao wakinunua ‘wanapiga kimya’. Kwa mfano msimu uliopita wamenunua kahawa kutoka kwa baadhi yetu, lakini hawajatoa malipo ya pili na hatujui kama wana mpango huo,” Mkulima kutoka kijiji cha Muriba anasema, kwa sharti la kutotajwa jina.

Anaongeza “Kitendo cha wanunuzi binafsi kukwepa kupitia kwenye AMCOS na kwenda moja kwa moja kununua kahawa kwa wakulima siyo kizuri, maana kinaikosesha Serikali mapato.”

Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwatafuta wanunuzi binafsi wa kahawa kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo.

Meneja Mkuu wa WAMACU, Gisiboye, anabainisha kuwa wamepandisha bei ya kununua kahawa kutoka Sh 1,200 msimu uliopita hadi Sh 1,600 kwa kilo moja msimu huu na wananunua kwa ‘cash’.

Anasisitiza kuwa lengo la ushirika huo ni kuinua mkulima, ndiyo maana inanunua kahawa kwa ‘cash’ kupitia AMCOS, kisha kuwalipa wakulima malipo ya pili kutokana na faida iliyopatikana.


GM Gisiboye akizungumza na Mana Online News ofisini kwake

GM Gisiboye anafafanua kuwa katika msimu uliopita WAMACU ilinunua kilo 282,517 sawa na tani 282 za kahawa, kwa bei ya Sh 1,200 kwa kilo moja, kwa gharama ya Sh milioni 339, na hivi karibuni imewalipa malipo ya pili - kiasi cha Sh milioni 113, kwa bei ya Sh 400 kwa kila kilo moja.

Malipo hayo ya pili yanafanya bei ambayo WAMACU imetoa katika ununuzi wa kahawa msimu uliopita kufikia Sh 1,600 kwa kilo moja.

Kwa mujibu wa Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Kanda ya Ziwa, Mike Granta, WAMACU ndiyo imeongoza kwa kutoa bei nzuri ya malipo ya pili kwa wakulima wa kahawa, kuliko vyama vyote vya ushirika nchini katika msimu uliopita.

Wakati huo huo, WAMACU imetumia Sh milioni 99 kuzalisha vitalu vya miche 120,000 ya kahawa na Sh milioni 21 kulipia miche 42,000 ya zao hilo kwenda kwa wakulima.

“Tumezalisha vitalu vya miche hiyo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI),” GM Gisiboye anasema.

Kwa mujibu wa meneja huyo, hivi karibuni WAMACU imeidhinishiwa mkopo wa Sh milioni 980 kutoka TADB, na tayari imeshapokea Sh milioni 550 kwa ajili ya kuendesha shughuli zake, zikiwemo za kukusanya kahawa kupitia AMCOS.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages