NEWS

Tuesday 31 August 2021

MISA Tanzania kuwajengea wanahabari 400 uwezo wa kuhamasisha mabadiliko ya sheria za habari



TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inakusudia kuwafikia waandishi wa habari zaidi ya 400, kupitia mradi wa kuwajengea uwezo wa kushiriki katika kuhamasisha mabadiliko ya sheria na sera za habari, kwa ustawi wa sekta ya habari nchini.

Akizungumza na Mara Online News muda mfupi baada ya mafunzo hayo ya siku moja kwa waandishi wa habari 35 kutoka vyombo mbalimbali vya habari mkoani Mara katika Hoteli ya Mativilla Beach mjini Musoma jana Agosti 30, 2021, Afisa Habari wa MISA Tanzania na Mratibu wa mradi huo, Jacqueline Jones amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa Mei mwaka huu mkoani Morogoro.


Jacqueline Jones akizungumza na Mara Online News

Jones amefafanua kuwa mradi huo ni wa miaka miwili na unatekelezwa kwa ushirikiano wa MISA Tanzania na taasisi ya Kimataifa ya Kusaidia Vyombo vya Habari (IMS), chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Ametaja sheria zenye vikwazo dhidi ya utendaji kazi wa waandishi wa habari nchini kuwa ni Sheria ya Mawasiliano (EPOCA) ya Mwaka 2010, Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari (MSA) ya Mwaka 2016 na Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2019.


Wanahabari wa mkoani Mara wakishiriki mafunzo hayo

Mafunzo hayo yamejikita katika kuwaelimisha waandishi wa habari sheria hizo na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika kuhamasisha mabadiliko ya vipengele visivyo rafiki kwa utendaji wa kazi zao za kitaaluma.

“Tunataka waandishi wa habari washiriki kwani wamekuwa nyuma katika ushiriki wa kuhamasisha mabadiliko ya sheria hizo. Mabadiliko hayo ni muhimu kwa manufaa ya umma,” Jones amesema.

Washiriki wakifuatilia mada katika mafunzo hayo


Washiriki wakiendelea na mafunzo

Jones amesisitiza kuwa Misa Tanzania ingependa kuona waandishi wa habari wa Tanzania wakipigania kupata sheria ambazo ni rafiki kwa uhuru wa vyombo vya habari na wa kutoa maoni kwa manufaa ya taifa.

Ameongeza kuwa vifungu vya sheria visivyo rafiki kwa wanahabari vikirekebishwa vitasaidia pia kuwawajibisha viongozi na watendaji wa umma, kwa manufaa na maendeleo ya taifa.

Sehemu nyingine ya washiriki

“Ajenda kubwa hapa ni kupata sheria ambazo zinatoa huru wa kupata habari na uhuru wa vyombo vya habari (access to information and freedom of press).

“Wito wangu kwa waandishi wa habari ni kuwa wa- personalize (wajivishe) hii movement (hatua) na kuona umuhimu wa wao kushiriki,” Jones amesisitiza.


Washiriki wa mafunzo wakijadiliana kundini

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, mkoa wa Mara ni wa tatu kupata mafunzo hayo, ukitanguliwa na mikoa ya Morogoro na Tanga.

Amebainisha kuwa hadi sasa wameshaendesha mafunzo hayo kwa waandishi wa habari 105 katika mikoa hiyo, kwa maana ya 35 katika kila mkoa.

Hata hivyo, Jones ametaja changamoto wanazokutana nazo wakati wa mafunzo hayo kuwa ni pamoja na waandishi wa habari wengi kusema hawana maamuzi kwenye vyombo vyao vya habari. “Sera za vyombo vya habari nazo ni changamoto,” amesema.


Washiriki wengine wa mafunzo hayo wkijadiliana kundindi

Mafunzo hayo ya mkoani Mara yamehitimishwa kwa washiriki kuainisha namna watakavyotumia taaluma yao kuhamasisha mabadiliko ya sheria na sera za habari zisizo rafiki kwa waandishi wa habari nchini.

“Tumejadiliana na wenyewe wamekuja na commitments (ahadi) zao jinsi watakavyoshiriki katika kuhamasisha marekebisho ya sheria hizi ambazo zinakwaza utendaji wao, ili kujenga mstakabali mzuri wa sekta ya habari hapa nchini,” Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Jesse Kwayu amesema.


Kwayu akiwezesha mafunzo hayo

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages