NEWS

Sunday 1 August 2021

Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation apata ajali Serengeti

Gari lililopata ajali

MKURUGENZI wa Taasisi ya Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera na watu wengine wawili, wamepata ajali ya gari katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Meneja wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na taasisi hiyo, Frank Joashi ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo asubuhi, kwamba ajali hiyo ilitokea jana Julai 31, 2021 saa mbili asubuhi baada ya gari lenye namba za usajili T 127 AKQ walilokuwa wakisafiria kuanguka mtoni.

Kwa mujibu wa Joash, gari hilo lilikuwa limebeba watu watatu, akiwemo yeye na kwamba wote walinusurika.

"Tupo salama japo Hezbon ndiye ameumia sana na tupo njiani kuelekea Bugando - Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi," amesema.

Ameshukuru wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kutoa msaada wa haraka mara tu baada ajali hiyo kutokea.

"Wafanyakazi wa Hifadhi ya Serengeti walikuwa watu wa kwanza kufika eneo la ajali kwa wakati na kufanya uokozi, kisha kutupatia msaada wa kutupeleka Hospitali ya DDH Mugumu. Tunawashukuru sana tena mwendo ulikuwa mzuri na hakukuwa na ucheleweshaji,” Joashi amesema.

Hezbon Peter Mwera

Kwa mujibu wa Joashi, walipata ajali hiyo wakati wakielekea kutembelea hoteli za kitalii zilizopo ndani ya hifadhi hiyo kutafuta nafasi za masomo ya vitendo (field), kwa ajili ya wanafunzi wa chuo chao.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Masana Mwishawa amesema hifadhi ilitoa msaada wa haraka baada ya kupata taarifa za tukio hilo.

“Kama Hifadhi tunatoa pole sana kwao, tuliwachukua na kuwapeleka hospitali kwa matibabu,” Mwishawa ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo.

Hata hivyo, habari zilizotufikia hivi punde zinasema Hezbon anasafirishwa leo kwenda Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza, kwa matibabu zaidi.

Wakati huo huo, Mhifadhi Mwishawa amesema Hifadhi ya Serengeti inafanya juhudi za kulitoa gari lilopata ajali mtoni, ili kulipeleka eneo la Seronera hifadhini, kwa usalama.

Mara Online News inaendelea na juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, kwa ajili ya kuzungumzia ajali hiyo, ambayo chanzo chake bado hakijafahamika.

MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages