NEWS

Friday 17 September 2021

Bilioni 68 zilizotolewa na Ujerumani zitakavyosaidia uhifadhi Serengeti, Katavi na Mahale
MAGEUZI makubwa yanatarajiwa kuonekana katika Hifadhi za Taifa za Serengeti, Katavi na Mahale, baada ya Ujerumani kuipatia Tanzania Sh bilioni 68 kwa ajili ya kuziimarishia shughuli za uhifadhi.

Mpango huo umethibitishwa na viongozi wa serikali za mataifa hayo waliosaini mikataba mitatu ya utekelezaji, katika hafla maalum iliyofanyika Seronera, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Septemba 14, 2021.

Waliohusika kusaini mikata hiyo ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW), Jennifer Woerl, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Jenerali Mstaafu George Waitara na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Allan Kijazi.


Jennifer Woerl (wa pili kushoto) akisaini mkataba


Dkt Kijazi (kushoto) akisaini mkataba

Wamesaini mikataba hiyo mbele ya Mkurugenzi wa Masuala ya Afrika kutoka Serikali ya Ujerumani, Dkt Stefan Oswald na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, miongoni mwa viongozi wengine.


Nibu Waziri Masanja (kulia) na Dkt Oswald wakionesha nakala ya mojawapo ya mikataba iliyosainiwa.

Naibu Waziri Masanja, Dkt Kijazi na Jenerali Mstaafu Waitara kwa nyakati tofauti wameishukuru Serikali ya Ujerumani wakisema msaada huo umekuja wakati mwafaka, kwani TANAPA imeyumba kimapato kutokana na mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19) uliotikisa dunia na kuathiri sekta ya utalii.

Dkt Oswald na Woerl wamesema Ujerumani imetoa msaada wa fedha hizo kutokana na kuridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuendeleza uhifadhi wa wanyamapori.


Dkt Oswald (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla hiyo

Wameongeza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuendeleza uhusiano na urafiki wa muda mrefu (miaka 60) sasa baina ya Ujerumani na Tanzania, ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mkurugenzi wa zamani wa Shirika la Uhifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) la Ujerumani, Profesa Bernhard Grzimek.Naibu Waziri Masanja ameishukuru Serikali ya Ujerumani akisema fedha hizo zitasaidia kuimarisha miradi ya uhifadhi wa mifumo ya ikolojia katika hifadhi husika.

Miradi hiyo itatekelezwa na TANAPA kwa kushirikiana na FZS, ambapo kati ya Sh bilioni 68 zilizotolewa na Ujerumani, bilioni 46 zinaelekezwa katika Hifadhi za Taifa za Katavi na Mahale na bilioni 22 ni kwa ajili ya Hifadhi ya Serengeti.

Miradi hiyo ni ya miaka mitano kwa Hifadhi za Taifa za Katavi na Mahale, na miaka miwili kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji akizungumza katika hafla hiyo.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Dkt Kijazi amesema kuwa mbali na uimarishaji wa shughuli za uhifadhi, fedha hizo zitasaidia pia kugharimia kampeni ya uboreshaji wa uhusiano kati ya hifadhi hizo na wakazi wa vijiji vinavyopakana nazo.

Amebainisha kuwa eneo linalolengwa zaidi katika Hifadhi za Taifa za Katavi na Mahale ni ushoroba unaounganisha hifadhi hizo.


Dkt Kijazi (kushoto) akizungumza

“Idadi kubwa ya soko wanatumia eneo linalounganisha hifadhi hizi, hivyo msaada huu utasaidia kushirikisha jamii katika utunzaji na ulinzi wa ikolojia ya ushoroba huo,” Dkt Kijazi amesema.

Kwa upande wa Serengeti, amesema fedha hizo zitasaidia kugharimia shughuli za ulinzi wa hifadhi na kampeni ya kuimarisha uhusiano kati yake na wakazi wa vijiji jirani katika wilaya za Serengeti, Bunda, Tarime na Bariadi na Ngorongoro.

Naye Jenerali Mstaafu Waitara amesema fedha hizo zitasaidia pia kuboresha miundombinu katika hifadhi hizo na uendeshaji wa TANAPA.


Jenerali Mstaafu Waitara akisaini mkataba

Siku moja kabla ya mikata hiyo kusainiwa, Dkt Oswald ameongozwa na Naibu Waziri Masanja kukagua maendeleo ya miradi ya uhifadhi inayotekelezwa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ushirikiano na Shirika la Uhifadhi la FZS katika hifadhi hiyo.

Miradi hiyo ni pamoja na karakana ya Seronera, zana za kupambana na ujangili na chumba maalumu cha masuala ya operesheni za hifadhi.

Pia wametembelea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) ya IKONA ambapo walizungumza na viongozi wa husika.Viongozi wengine walioshiriki ziara hiyo ni Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema, Kamishna Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa TANAPA, Pascal Shelutete.

Wengine ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Masana Mwishawa, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji, Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George na Meneja Mradi wa FZS Serengeti, Masegeri Rurai.

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages