NEWS

Thursday 30 September 2021

Fahamu nchi zinazoongoza kusoma Mara Online News 
BLOGU ya Mara Online News inatembelewa na kusomwa na maelfu ya watu wa mataifa mbalimbali, huku Tanzania ikiongoza kwa kuwa na wasomaji zaidi ya 110,000.

Takwimu za blogu hiyo za wiki hii zinaonesha kuwa Tanzania inafuatiwa na nchi ya Hong Kong yenye wasomaji zaidi ya 23,000, Indonesia (zaidi ya 18,000) na Israel (zaidi ya 11,000).

Nchi nyingine ni Marekani, Ubelgiji, Uholanzi, China, Ujerumani, Kenya, Urusi, Ufaransa, Japan, India, Uingereza, Uganda, Norway na nchi za Uarabuni, ambazo kila moja ina wasomaji kati ya 10,000 na 4,000.
 
“Tumejipanga vizuri kuendelea kuwapatia wasomaji wetu habari bora na za uhakika na sio kurusha kila kitu kwenye mtandao.


“Tungependa kuwa sehemu ambayo wasomaji wakiingia wanasoma habari zenye kuonesha fursa katika sekta mbalimbali, huku suala la uhifadhi wa wanyamapori, vyanzo vya maji na mazingira likiwa moja ya vipaumbele vyetu.

“Hiki sio chombo cha kuweka habari za kukatisha wasomaji wetu tamaa, au kuwafanya wahuzunike. Huo ndio uelekeo wetu na tunawashukuru sana wasomaji wetu kwa kuendelea kusoma blogu yetu na gazeti letu la Sauti ya Mara linalotoka kila wiki,” Mhariri Mtendaji na mwanzilishi wa vyombo hivyo vya habari, Jacob Mugini anasema.


Jacob Mugini akizungumzia maendeleo ya blogu ya Mara Online News.

Anaongeza kuwa Mara Online News pia wana akaunti ya twitter inayochapisha matukio mapya kuhusu uhifadhi na maji, kwa lugha ya Kiingereza, yenye ina wanachama wa ndani na nje ya nchi, yakiwemo mashirika ya kimataifa yanayojihusisha na uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji.

Mashirika hayo ni pamoja na chuo maji cha IHE Delft kilichopo chini ya UNESCO nchini Uholanzi, Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (LUPC) miongoni mwa mengine.
“Watalamu wa masuala ya maji na uhifadhi wamekuwa waki- ‘retweet updates’ zetu ndani na nje ya nchi, na wengi ni ambao wanaunga mkono uhifadhi wa vyanzo vya maji, ukiwemo Mto Mara,” Mugini anasema.

Blogu ya Mara Online News ni chombo dada cha habari cha Gazeti la Sauti ya Mara, vilivyosajiliwa serikalini, vyote vikimilikiwa na Mara Online.
Blogu ya Mara Online News ilizinduliwa rasmi Desemba 15, 2020 na Adam Malima akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, kabla ya kuhamishiwa mkoa wa Tanga, na Gazeti la Sauti ya Mara lilizinduliwa Januari 2020.

Vyombo hivyo vimejikita katika kuchapisha habari na makala zinazohamasisha uhifadhi na utunzaji endelevu wa vyanzo vya maji, wanyamapori, mazingira hai, maendeleo ya elimu, kilimo, madini, uvuvi, uwekezaji wa viwanda na usawa wa kijinsia.


Kushoto ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete (kushoto) na Mugini wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa blogu ya Mara Online News.

Blogu ya Mara Online News na Gazeti la Sauti ya Mara vinaendeshwa na waandishi wa habari na wahariri waandamizi nchini, Jacob Mugini (Mhariri Mtendaji) na Christopher Gamaina (Mhariri Mkuu).


Christopher Gamaina (kushoto) akifanya mahajiano na mhifadhi.

Wahariri hao ni waandishi wa habari wenye ubobezi katika kukusanya na kuchakata habari kwa miaka 18 sasa.


Mugini akifanya mahojiana na Mama Graca Machel

Mugini ni mwandishi wa habari (news stories) na makala (feature articles) kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza, huku akijikita kwenye kuandika habari za uhifadhi, maji, kilimo, elimu na madini.
Wamekuwa wakifanya kazi na waandishi ambao ni wahitimu kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, vikiwemo UDOM na SAUT.


Mugini akiwa katika mafunzo ya mobile reporting jijini Dar es salaam.

Mwaka 2011 Mugini aliibuka mshindi wa mafunzo ya kuripoti habari za mtandao, kwa kutumia simu za mkononi (mobile reporting) yaliyotolewa na shirika la Voices of Media Foundation la Uholanzi, kupitia Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF).

Baada ya kuibuka mshindi, Mugini alipata fursa ya kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ndani na nje ya Tanzania.
Mwaka huo huo , Mugini alihudhuria mkutano wa dunia wa vyombo vya habari( Global Media Forum) uliofanyika Bonn, Ujerumani na kuwa mmoja wa wazungumzaji, kisha kuwenda nchini Uholanzi ambapo alihudhuria mafunzo ya kuandika habari za watoto, yaliyofanyika The Hague.


Mwaka 2019, Mugini pia alipata fursa ya kuhudhuria mafunzo ya kuripoti habari za maji katika mji wa Delft nchini Uholanzi, ambapo alikutana na waandishi wengine 18 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, chini ya uhafdhili wa Serikali ya Uholanzi. Mafunzo hayo yalifanyika katika chuo cha maji cha Delft kinachomilikiwa UNESCO.
Hadi sasa vyombo vya habari vya Mara Online News na Sauti ya Mara vimendelea kuvutia wadau wa masuala ya maji, mazingira na uhifadhi kutoka ndani na nje ya nchi.


Naye Gamaina, mbali na uzoefu wa kuwa mhariri wa vyombo mbalimbali nchini, yakiwemo magazeti ya Jamhuri jijini Dar es Salaam, Mtanzania, Raia Mwema, Raia Tanzania na sasa Sauti ya Mara na Mara Online News Kanda ya Ziwa, Mei 2017 alitunukiwa tuzo baada ya kuibuka Mshindi wa Kwanza wa Kundi la Uandishi wa Habari za Takwimu (Data Journalism Category) kwenye mashindano ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2016, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Waandishi wa Mara Online kazini

(Habari na Asteria John)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages