NEWS

Wednesday 29 September 2021

RC Hapi atimiza ahadi ya Sh milioni 10 kwa Biashara United




MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Salum Hapi ameikabidhi timu ya Biashara United ya mkoa huo, kitita cha shilingi milioni 10, alizoiahidi baada ya kutoka sare katika mchezo dhidi ya Simba ya Dar es Salaam.

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Uwekezaji uliopo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma, leo Septemba 29, 2021.

RC Hapi amesema uongozi wa mkoa wa Mara umejipanga kuiboresha timu hiyo, ili iweze kufanya vizuri katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Kwa sasa tunafanya mazungumzo na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuidhamini timu ya Biashara United kwa udhamini mkubwa zaidi wenye thamani ya zaidi ya bilioni moja msimu huu,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa udhamini huo, Biashara United itakuwa na uhakika wa fedha za kujiendesha, ikiwa ni pamoja na mishahara ya wachezaji na usafiri wa timu katika kushiriki mechi mbalimbali.

RC Hapi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Timu ya Biashara United, ameipongeza timu hiyo kwa mchezo mzuri walioonesha na kuiwezesha kupata sare katika mechi yake dhidi ya Simba.

Pia, amewapongeza wachezaji kwa mafanikio waliyopata msimu uliopita na mechi mbili walizocheza nje ya nchi, ambapo Biashara United ilifanya vizuri.

Amewataka wachezaji kuongeza ari ya kujitolea kuinyanyua timu hiyo iweze kupata ubingwa msimu huu, ili pia iwe rahisi kupata udhamini tena miaka inayofuata.

Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amempongeza golikipa wa Biashara United, Ssetuba James Cleo, kwa jitihada kubwa alizofanya katika mechi hiyo, ikiwa ni pamoja na kudaka mpira wa penati iliyopigwa na mchezaji wa Simba.

Ameeleza kuwa kabla ya mechi hiyo, alitoa ahadi kwamba yeye na wapenzi wa Biashara United wangetoa shilingi milioni 15 kama B ingeshinda, na shilingi milioni 10 kama ingetoka sare.


RC Hapi (kushoto) akikabidhi kitita hicho kwa mwakilishi wa Biashara United.

“Katika fedha nilizokabidhi leo, wachezaji wote 31 wa Biashara United watapata shilingi laki tatu kila mmoja na fedha inayobakia itagawiwa kwa benchi la ufundi,” RC Hapi amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Timu ya Biashara United, Selemani Mataso amemshukuru RC Hapi kwa kutekeleza ahadi yake, ambayo imewapa hamasa na kuwajengea ari wachezaji wa timu hiyo.

“Mwaka huu tumeisajili timu vizuri sana, tunasubiri vibali tu vya baadhi ya wachezaji wetu, vikipatikana tunaweza kufanya vizuri zaidi. Ubingwa unakuja Mkoa wa Mara msimu huu,” Mataso amesema.

Ameeleza kuwa kwa sasa vipaumbele vyao ni kuona timu inawalipa wachezaji stahiki zao kwa wakati, huku akimpongeza mwalimu wao kwa kazi kubwa anayofanya kuwaimarisha katika mazoezi.

Mechi ya Simba na Biashara United imefanyika jana Septemba 28, 2021 katika Uwanja wa Karume uliopo katika Manispaa ya Musoma, ambapo timu zilitoka sare ya bila kufungana.

Katika msimu uliopita wa 2021/2022, Biashara United ilidhaminiwa na Mgodi wa North Mara kwa shilingi milioni 350 na Kiwanda cha Jamakaya cha Shinyanga kwa shilingi milioni 100 na wengine waliokuwa wanadhamini baadhi ya mahitaji ya timu hiyo, na ilifanikiwa kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

(Na Mwandishi wa Mara Online, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages