NEWS

Thursday 7 October 2021

Watoto wote barani Afrika kupewa chanjo ya Malaria


Watoto kote barani Afrika watapewa chanjo dhidi ya malaria katika hatua ya kihistoria kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.
Malaria imekuwa moja ya janga kubwa kwa wanadamu kwa milenia na inaua zaidi watoto wachanga.

Kuwa na chanjo - baada ya zaidi ya karne ya kujaribu - ni kati mojawapo ya mafanikio makubwa katika tasnia ya tiba.


Chanjo hiyo - inayoitwa RTS, S - ilithibitishwa kuwa na ufanisi miaka sita iliyopita.

Sasa, baada ya kufanikiwa kwa mipango ya chanjo ya majaribio nchini Ghana, Kenya na Malawi, Shirika la Afya Ulimwenguni linasema chanjo hiyo inapaswa kusambazwa kote Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika maeneo mengine yenye maambukizi ya wastani na ya juu ya ugonjwa wa malaria.

Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkurugenzi mkuu wa WHO, alisema ni "wakati wa kihistoria".

"Chanjo ya malaria inayosubiriwa kwa muda mrefu kwa watoto ni mafanikio ya sayansi, afya ya mtoto na udhibiti wa malaria," alisema. "[Inaweza] kuokoa makumi ya maelfu ya maisha ya watoto kila mwaka."

Vimelea Hatari

Malaria ni vimelea ambavyo huvamia na kuharibu seli zetu za damu ili kuzaliana, na huenezwa na kuumwa na mbu wanaonyonya damu.

Dawa za kuua vimelea, vyandarua vya kuzuia kuumwa na wadudu hao vimesaidia kupunguza malaria.

Lakini mzigo mkubwa wa ugonjwa umeliathiri bara la Afrika, ambapo zaidi ya watoto 260,000 walikufa kutokana na ugonjwa huo mnamo 2019.

Inachukua miaka kadhaa ya kuambukizwa mara kwa mara ili kujenga kinga na hata hii inapunguza tu uwezekano wa kuwa mgonjwa sana.

Dk Kwame Amponsa-Achiano alijaribu chanjo hiyo nchini Ghana kutathmini ikiwa chanjo ya ya watu wengi pamoja ilikuwa inaweza kupata ufanisi.

"Ni jambo la kufurahisha sana kwetu, na chanjo kwa watu wengi ninaamini idadi ya malaria itapunguzwa kwa kiwango cha chini kabisa," alisema.

Kuambukizwa malaria kila wakati kama mtoto kulimchochea Dk Amponsa-Achiano kuwa daktari huko Ghana.

"Ilikuwa hatua ya kusikitisha, karibu kila wiki ulikuwa nje ya shule, malaria imetuangamiza kwa muda mrefu," aliniambia.

Kuokoa Maisha ya Watoto

Kuna aina zaidi ya 100 ya vimelea vya malaria. Chanjo ya RTS, S inalenga ikle ambacho ni hatari zaidi na cha kawaida barani Afrika: Plasmodium falciparum.

Majaribio, yaliyoripotiwa mnamo 2015, yalionyesha chanjo hiyo inaweza kuzuia karibu kesi nne kati ya 10 za malaria, tatu kati ya kesi 10 kali na kusababisha idadi ya watoto wanaohitaji kutiwa damu ikipungua kwa theluthi.

Walakini, kulikuwa na mashaka chanjo hiyo ingefanya kazi kwani inahitaji dozi nne kuwa na ufanisi . Tatu za kwanzahutolewa moja baada ya kila mwezi katika miezi ya tano , sita na saba, na nyongeza ya mwisho inahitajika karibu na miezi 18.


Matokeo ya majaribio ya mwanzo yalijadiliwa na vikundi viwili vya wataalam katika WHO mnamo Jumatano.

Matokeo, kutoka kwa dozi zaidi ya milioni 2.3, yalionyesha:

• Chanjo ilikuwa salama na bado ilisababisha kupunguzwa kwa malaria kali kwa asilimia 30%

• Ilifikia zaidi ya theluthi mbili ya watoto ambao hawana chandarua cha kulala ndani

• Hakukuwa na athari mbaya kwa chanjo zingine za kawaida au hatua zingine za kuzuia malaria

• Chanjo ilikuwa ya gharama nafuu

"Kwa mtazamo wa kisayansi, haya ni mafanikio makubwa, kutoka kwa mtazamo wa afya ya umma hii ni hatua ya kihistoria," alisema Dk Pedro Alonso, mkurugenzi wa Programu ya Malaria ya Ulimwenguni katika shirika la WHO.

"Tumekuwa tukitafuta chanjo ya malaria kwa zaidi ya miaka 100 sasa, itaokoa maisha na kuzuia magonjwa kwa watoto wa Kiafrika."

Kwa nini ni vigumu kukabiliana na malaria ?

Baada ya kushuhudia ulimwengu ukiunda chanjo za Covid katika muda wa mfupi zaidi , unaweza kujiuliza ni kwanini imechukua muda mrefu kuunda chanjo ya malaria?

Malaria husababishwa na vimelea ambavyo ni vya kipekee na vinavyobadilika zaidi kuliko virusi vinavyosababisha Covid. Kulinganisha viwili hivyo ni kama kulinganisha mtu na kabichi.

Vimelea vya malaria vimebadilika ili kukwepa mfumo wetu wa kinga. Ndio maana lazima upate malaria mara kwa mara kabla ya kuanza kupata kinga hata kidogo.

Ina hali na mifumo migumu kuelewa katika spishi mbili (wanadamu na mbu), na hata ndani ya mwili wetu ina tabia sugu kwani inaambukiza seli za ini na seli nyekundu za damu.

Kuunda chanjo ya malaria ni kama kupigilia jeli kwenye ukuta na RTS, S ina uwezo tu wa kulenga fomu ya sporozoite ya vimelea (hii ni hatua kati ya kung'atwa na mbu na vimelea kufika kwenye ini).

Ndio sababu chanjo ina '40% tu ya ufanisi. Walakini, hii bado ni mafanikio ya kushangaza na inapeana njia ya ukuzaji wa chanjo zenye nguvu zaidi.

Chanjo hiyo, iliyotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya GSK, haitachukua nafasi ya hatua zingine zote za kudhibiti malaria kama vile vyandarua vilivyotibiwa na dawa za kuua wadudu.

Itatumika pamoja nazo ili kuafikia lengo la kuzuia kabisa vifo vinavyotokana na malaria.

Na haitatumika nje ya Afrika ambapo aina tofauti za malaria, ambazo chanjo haiwezi kulinda dhidi yake, zimeenea zaidi.

Dr Ashley Birkett, kutoka mpango wa chanjo ya malaria wa Path, alisema kuzindua chanjo hiyo ni "tukio la kihistoria" ambalo "litaondoa hofu" kutoka kwa familia.

Aliniambia: "Hebu fikiri kuhusu mtoto wako mchanga anayeweza kuwa mzima siku moja na amejaa uwezo halafu baada ya kuumwa na mbu aliyeambukizwa, wakati akicheza na marafiki au kulala kitandani, anaweza kufa katika wiki kadhaa.

"Malaria ni shida kubwa, inaogofya na kutisha."

Chanzo: BBC News

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages