NEWS

Thursday 7 October 2021

Mtanzania ashinda Tuzo ya Nobel kuhusu Fasihi 2021

Mwandisi wa riwaya nchini Tanzania, Abdulrazak Gurnah ametuzwa Tuzo ya Amani ya Nobel kuhusu Fasihi 2021.

Akimtangaza kuwa mshindi siku ya Alhamisi, kituo kinachotoa tuzo hizo kilimpongeza Gurnah kwa kuangazia suala la ukoloni na athari zake katika utunzi wake.

Tuzo hiyo inayotolewa na kituo hicho cha Sweden ina thamani ya corona milioni kumi za taifa hilo sawa na Dola  milioni 1.14 au pauni 840,000.
Gurnah mwenye umri wa miaka 73 ni mwandishi wa riwaya 10 , ikiwemo Paradise na Desertion.

Riwaya ya Paradise iliochapishwa 1994, inaangazia hadithi ya mvulana aliyekulia nchini Tanzania katika karne ya 20 na kushinda tuzo ya Booker na hivyobasi kuanza kupata ufanisi wake kama mwandishi wa Riwaya.

'Tamaduni na mabara'

"Kujitolea kwa Abdulrazak Gurnah katika kuangazia ukweli na masuala mengine kwa urahisi bila kuchukiza kunashangaza'' , ilisema kamati ya tuzo ya Nobel kuhusu fasihi katika taarifa yao.

"Riwaya zake zimetungwa kufuta maelezo ya uwongo na kuyafungua macho yetu kwa Afrika Mashariki iliojaa tamaduni tofauti ambazo hazijulikani katika sehemu nyengine za ulimwengu."
Vitabu vilivyoandikwa na Gurnah vikiwa katika maonesho.
"Wahusika [wake] hujikuta katika hali ya kutatanisha kati ya tamaduni na mabara, kati ya maisha ya awali na maisha yanayoibuka; ni hali isiyoweza kutatuliwa kamwe."

Akiwa mzaliwa wa Zanzibar mwaka 1948, Gurnah aliwawasili nchini Uingereza akiwa mkimbizi mwisho wa miaka ya sitini.

Alikuwa profesa wa riwaya za Kiingereza na riwaya za baada ya ukoloni katika chuo kikuu cha Kent , Cantebury hadi alipostaafu hivi karibuni.

Gurnah ni Mwafrika wa kwanza mweusi kushinda tuzo hiyo tangu Wole Soyinka . Katika mahojiano 2016 , alipoulizwa iwapo angejiita mwandishi wa riwaya za baada ya ukolini au riwaya za dunia, Gurnah alijibu : nisingetumia maneno haya nisingependa kujiita mwandishi wa aina yoyote.

Ukweli ni kwamba sidhani kama ningejiita jina jingine lolote zaidi ya jina langu. Nadhani iwapo mtu angeniuliza , ingekuwa njia nyengine ya kusema , Je wewe ni mmoja kati ya haya..? Kwa kweli ningesema hapana!. Nisingependelea kuwa na jina zaidi.

Tuzo za Nobel , ambazo zimetuzwa tangu 1901 , zinatambua ufanisi katika fasihi , sayansi , amani na uchumi.

Washindi wa awali wanashirikisha waandishi wa Riwaya kama vile Ernest Hemingway, Gabriel Garcia Marquez na Toni Morrison, washairi kama vile Pablo Neruda, Joseph Brodsky na Rabindranath Tagore, na waandishi wa michezo ya kuigiza akiwemo Harold Pinter na Eugene O'Neill.

Aliyekuwa waziri mkuu wa zamani nchini Uingereza Winston Churchill alishinda kwa kumbukizi yake , Bertrand Russell kwa filosofia yake na Bob Dylan kwa mishororo yake.

Tuzo ya mwaka uliopita ilichukuliwa na mshairi wa Marekani Louise Gluck.

CHANZO: BBC News

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages