NEWS

Monday 18 October 2021

Musoma Vijijini wajenga zahanati mpya 16 kwa mpigo, wasubiri fedha za IMF kuzikamilisha




WANANCHI wa jimbo la Musoma Vijijini katika mkoa wa Mara wana kila sababu ya kumegewa sehemu ya Sh bilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kugharimia kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 nchini.
 
Oktoba 11, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan amezindua kampeni hiyo jijini Dodoma na kuelekeza fedha hizo zitumike kugharimia uboreshaji wa huduma za afya, elimu na maji.

Hakuna shaka kuwa wananchi wa Musoma Vijijini ni miongoni mwa walengwa wa fedha hizo, kwani zimekuja kipindi ambacho wamejizatiti kujenga zahanati mpya 16 zinazosubiri ukamilishwaji ili zianze kutoa huduma.

Zahanati hizo zimejengwa katika vijiji vya Buira, Busekera, Burungu, Butata, Bwai, Chimati, Chirorwe, Kakisheri, Kurukerege, Kurwaki, Maneke, Mkirira, Mmahare, Muhoji, Nyabaengere na Nyasaungu.


“Wachangiaji wakuu wa ujenzi wa zahanati hizi ni wanavijiji na viongozi wao, akiwemo Mbunge Profesa Sospeter Muhongo, madiwani na baadhi ya wazaliwa wa Musoma Vijijini,” Mmoja wa wasaidizi wa mbunge huyo, Varediana Mgoma ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu, hivi karibuni.

Mgoma ameongeza “Baadhi ya zahanati hizo zimepokea michango ya fedha kutoka Serikali Kuu. Halmashauri yetu ya Wilaya ya Musoma nayo inaombwa ianze kuchangia ujenzi huu.”

Ametaja miradi mingine mipya ya afya inayotekelezwa kuwa ni ujenzi wa wodi tatu za mama na mtoto katika zahanati za kisiwani Rukuba, Bukima na Nyegina. Pia ujenzi wa vituo vya afya vya Bugwema na Makojo kutokana na mchango mkubwa kutoka serikalini.



Pia, Hospital ya Wilaya inayojengwa na Serikali, ambapo kila kijiji kinachangia shilingi milioni mbili.

Aidha, katika juhudi za kuboresha huduma za afya jimboni, Mbunge Muhongo ameshatoa magari matano ya kubeba wagonjwa, ambayo hata hivyo kwa sasa yamechoka baada ya kutumika kwa muda mrefu.

Magari hayo yalipelekwa katika vituo vya afya Murangi na Mugango, zahanati za Kurugee, Masinono na Nyakatende.


“Kwa sasa wananchi na viongozi wa jimbo hili tunaomba michango ya fedha, zikiwemo zilizotolewa na IMF kwa ajili ya kugharimia ukamilishaji wa miundombinu ya zahanati mpya zilizojengwa jimboni.

“Vilevile tunaomba magari mawili ya kubeba wagonjwa kwa kuzingatia ukubwa wa jimbo hili,” Mbunge Muhongo amesema katika mazungumzo na Mara Online News kwa njia ya simu, hivi karibuni.

Kwa sasa jimbo la Musoma Vijijini lina zahanati 24 za Serikali na nne za binafsi, vituo vya afya viwili lilivyopo Murangi na Mugango na magari matano ya kubeba wagonjwa yaliyotolewa na mbunge huyo.

Kuhusu chanjo ya UVIKO-19, Mbunge Muhongo amesema wananchi wa jimbo hilo wanaendelea kujitokeza kupata chanjo katika vituo 28 na kwamba naye alishachanjwa.


Profesa Muhongo akichangia mjadala bungeni

“Wananchi wa jimbo la Musoma Vijijini wamekuwa na mwamuko mkubwa wa kujitolea kuanzisha na kutekeleza miradi ya maendeleo yao kwenye sekta mbalimbali, zikiwemo za afya, elimu, Kilimo, uvuvi, ufugaji, utamaduni na michezo.

“Lakini pia Serikali inatoa michango ya fedha kwenye utekelezaji wa baadhi ya miradi hiyo,” Profesa Muhongo amesema.

Jimbo la Musoma Vijijini linaundwa na kata 21 zenye vijiji 68 na vitongoji 374.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara, Oktoba 18, 2021

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages