NEWS

Sunday 17 October 2021

Mbunge Kembaki anavyodhihirisha uongozi wa vitendo Jimbo la Tarime Mjini




MBUNGE wa Tarime Mjini mkoani Mara, Michael Kembaki ameendelea kuchochea maendeleo ya wananchi kwa kutekeleza ahadi zake na kuchangia miradi ya kijamii katika jimbo hilo.

Mbunge Kembaki ameendelea kudhihirisha hayo katika ziara yake ya hivi karibuni ya kuhamasisha maendeleo ya wananchi, sambamba na kuchangia gharama za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii jimboni.

Sekta ya maji
Mojawapo ya ahadi zake, aliyotekeleza kwa vitendo ni uboreshaji wa kisima cha maji cha asili katika mtaa wa Mawasiliano, kwa gharama ya shilingi zaisi ya milioni mbili.


Mwanamke akipata huduma ya maji katika kisima cha asili kilichoboreshwa na Mbunge Kembaki

“Wakati naomba ridhaa ya kuwa mbunge, niliahidi kurekebisha kisima hiki ili muweze kupata maji safi, maana mvua ilikuwa ikinyesha maji yanageuka kuwa tope.

“Leo tunashuhudia kisiama hiki kikiwa katika mazingira mazuri, kitunzeni. Nimetimiza ahadi yangu, endeleeni kutumia maji, endeleeni kutuunga mkono, Mungu awabariki sana,” Kembaki amewambia wakazi wa eneo hilo wakati akikabidhi kisima hicho, hivi karibuni.


Mbunge Kembaki akikagua maji ya kisima hicho

Amesema visima vya asili lazima viendelezwe na kuimarishwa ili visaidie kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa jimbo la Tarime Mjini.

Aidha, Mbunge Kembaki amesema katika bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/2022, jimbo la Tarime Mjini limeidhinishiwa visima 11 vitakavyochimbwa ili kutatua changamoto ya huduma ya maji katika mji wa Tarime.

Amesema atashauriana na madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA) kwa ajili ya kupata maeneo yanayofaa kuchimbwa visima hivyo.

Kuhusu chanzo cha Nyandurumo kinachosambaza maji ya bomba mjini Tarime, Kembaki amesema “Nimeshawasilisha ombi kwa Waziri wa Maji, kwa ajili ya kujengewa chujio ili maji yawe safi na yanayotibiwa.”

Sekta ya elimu
Kwa upande wa elimu, Mbunge Kembaki amekabidhi msaada wa mashine ya kisasa ya ‘printer’ katika Shule ya Msingi ya Mazoezi Buhemba iliyopo kata ya Bomani.


Mbunge Kembaki akikabidhi printer hiyo

Amekabidhi msaada huo kwa uongozi wa shule hiyo wiki iliyopita, kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati wa mahafali ya wahitimu wa darasa la saba mwaka huu.

Afisa Elimu Kata ya Bomani, Thabita Kesowani na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Kordun Kivuyo wamemshukuru mbunge huyo na kuahidi kuitumia vizuri kwa maendeleo ya shule.

“Kupitia printer hii, tunatarajia ufaulu kuongezeka maradufu na tunapenda kumhakikishia mbunge kuwa hata mtihani uliofanyika hivi karibuni, ufaulu utaongezeka,” Mwalimu Kivuyo ameiambia Mara Online News, baada ya kupokea msaada huo.

Aidha, Mbunge Kembaki ameahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo yenye wanafunzi zaidi ya 1,500.

Kwa upande mwingine, Kembaki ameipatia shule ya msingi Kemahiri msaada wa saruji mifuko 50 na kuahidi kuelekeza fedha za mfuko wa jimbo katika kutatua changamoto ya madawati kwenye shule mbalimbali jimboni.


Pia, Mbunge Kembaki ameahidi kutoa shilingi milioni 10 kuchangia ununuzi wa eneo la kujenga shule ya msingi katika mtaa wa Gimenya katani Turwa.

“Natawachangia milioni 10, hapa naona panafaa, kwenye mitaa mingine eneo la nusu heka tu unaambiwa milioni sita, hapa ni zaya ekari nne, nampongeza huyu mwenye eneo ni mzalendo kweli kweli,” Mbunge Kembaki amesema.

Mwenyekiti wa mtaa huo, Nashon Samo amesema mitaa saba ilitakiwa kuchangia ununuzi huo, lakini mitatu imegoma na kwamba mwenye eneo hilo amekubali kuliuza kwa shilingi milioni 25.

Akarabati uwanja, atoa vifaa vya michezo
Mbunge Kembaki pia ametumia shilingi zaidi ya milioni mbili kugharimia ukarabati wa uwanja wa mpira wa miguu Serengeti uliopo mjini Tarime, uliokuwa hautumiki kwa muda mrefu na kukwamisha michezo wilayani hapa.

Katibu wa mbunge huyo, Elisha Samo amesema ofisi ya Mbunge Kembaki imegharimia ukarabati wa uwanja huo, baada ya kuombwa na wadau wa michezo, wakiwemo viongozi wa Chama cha Soka Tarime (TAFA).

“Mbunge ameilipa kampuni ya ujenzi KASCCO kiasi hicho cha pesa moja kwa moja kwenye akaunti yake kwa ajili ya kutawanya kifusi na kusawazisha uwanja huo, ambao pia ni muhimu kwa mikutano ya kijamii,” Samo amesema.

Pia, Mbunge Kembaki ametoa msaada wa jezi na mipira kwa timu 12 za soka za jimbo hilo.



Katibu wa mbunge huyo, Elisha Samo amekabidhi vifaa hivyo kwa wahusika, akiwa amefuatana na afisa michezo wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Teddy Msiangi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Malema Sollo.

Samo amesema msaada huo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Mbunge Kembaki katika kundeleza sekta ya michezo ndani ya jimbo hilo.

Baadhi ya timu zilizonufaika na msaada huo ni pamoja na Magoma, Boss Ruge, Bomani, Thadeo, Kilimo Sports Club, Kenyamanyori na Nyamwigwira.

Katibu wa TAFA, Sereria Marai amemshukuru Mbunge Kembaki akisema kukarabatiwa kwa uwanja huo, kumetoa fursa kwa ligi ya wilaya, ambayo tayari imeanza, baada ya kuahirishwa mara kadhaa kusubiri ukarabati.

Apiga marufuku ushuru umiza
Wakati huo huo, Mbunge Kembaki amepiga marufuku wajasiriamali kutozwa ushuru wa bidhaa wanazouza katika masoko ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Ametoa agizo hilo baada ya wajasiriamali wanaouza ndizi na dagaa katika soko la Tarime kumweleza kero hiyo, alipowatembelea, hivi karibuni.


Mbunge Kembaki (mwenye suti) akisalimia wajasiriamali sokoni

“Kuanzia leo natamka kwamba mkuu wa soko asitoze tena ushuru wowote, hadi pale kamati ya fedha na mipango ya halmashauri itakapokaa na kuamua vingenevyo,” Kembaki amesema na kushangiliwa na wajasiriamali hao.

Kembaki ametoa wito kwa wananchi wote wa jimbo la Tarime Mjini kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mifumo ya huduma za kijamii na kiuchuni nchini.

“Niinamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha ilani ya CCM inatekelezwa, tuendelee kumuunga mkono ili kazi iendelee,” Mbunge Kembaki amesema.


Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki (kulia), akisaidia wajasiriamali kuponda kokoto katika mtaa wa Gimenya jimboni, hivi karibuni.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara, Oktoba 11, 2021

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages