NEWS

Tuesday 12 October 2021

Siku ya Mtoto wa Kike: AICT Mara na Ukerewa yahamasisha haki za wasichana, ikiwemo kupata elimu bora



KANISA la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe limeshiriki maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, kwa kuhamasisha jamii kulinda haki za watoto wa kike, ikiwemo fursa sawa ya kupata elimu bora.

“Lakini pia mtoto wa kike anastahili haki ya kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kila aina,” Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota ameongeza.

Akisisitiza zaidi wakati wa maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyantira katika wilaya ya Tarime mkoani Mara jana, Bugota amesema kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha watoto wa kike wanapata mahitaji yao ya msingi.

“Watoto wa kike wanakutana na changamoto nyingi, wengi hawapewi fursa ya kupata elimu bora, wanakabiliwa na mila na desturi kandamizi, ndoa na mimba za utotoni, mambo ambayo yanasababisha wasifikie ndoto zao.

“Kwa hiyo jamii itambue kuwa watoto wa kike wanastahili kupewa fursa sawa, ikiwemo ya kupata elimu bora, lakini pia kupunguziwa majukumu ya nyumbani ambayo wakati mwingine yanawanyima muda wa kusoma.

“Tukiwapa watoto wa kike haki zao za msingi, ikiwemo ya kuwashirikisha katika maamuzi, tutawawezesha kuwa na sauti za kusikika na kupata haki zao,” Bugota amesisitiza.


Rebeca Bugota akizungumza katika maadhimisho hayo

Kwa mujibu wa Afisa Mradi huyo kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, kuwatimizia watoto wa kike haki zao za msingi, kutachangia ukuaji wa maendeleo na kupunguza umaskini katika jamii.

Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani mwaka huu - inayosema “Kizazi cha Kidijitali, Kizazi Chetu”, Bugota amesema inahamasisha jamii kuwapa watoto wa kike fursa sawa ya matumizi ya teknolojia na mitandao.

“Watoto wa kike wapewe fursa hiyo, kwani itawasaidia kusema changamoto zao, kujifunza vitu vingi, kuongeza uwezo utakaowawezesha kuwa wabunifu na kuliletea Taifa maendeleo,” amesema.



Naye Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwalimu Sophia Range, pamoja na kuishukuru AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kuandaa maadhimisho hayo katani kwake, amesema watoto wa kike wako katika kundi lenye mahitaji maalumu, hivyo wanahitaji uangalizi wa hali ya juu.

“Kwa mfano, kama mtoto wa kike atakuwa anatembea umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shule, anakuwa katika hatari ya kubakwa,” Mwalimu Range amesema.

Amewataka wazazi kushirikiana na wadau mbalimbali kuwajengea watoto wa kike dhana ya kujiamini kwamba wanaweza kufanya kazi yoyote kama watoto wa kiume.

“Tuwajengee watoto wa kike stadi ya kujiamini, na hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa tuna Rais mwanamke [Rais Samia Suluhu Hassan]. Kwanini wao wasifikirie kwamba baada ya Samia na wao wanaweza kuchukua uongozi.

“Rais Samia ameonesha kwamba hata wanawake wanaweza. Wazazi tuwape watoto fursa za kutosha, tuwajali wanaporudi nyumbani kutoka shule tusiwape kazi nyingi. Lakini pia Tusiwakekete, badala yake tuwape elimu ili tupate maprofesa wa kike, madaktari na wataalamu wengine,” Mwalimu Range ameongeza.


Mwalimu Sophia Range akiongoza jambo katika maadhimisho hayo

Afisa Elimu Kata huyo ameungwa mkono na Mwalimu Mary Mwita wa darasa la awali na kocha katika Shule ya Msingi Nyansincha, ambaye amekiri kuwa mtoto wa kike amekuwa akisahaulika, hasa katika haki ya kupata elimu bora kama mtoto wa kiume.

“Rais wetu [Rais Samia Suluhu Hassan] ni mwanamke na anaongoza vizuri, ni mfano kuwa wanawake wakiwezeshwa wanaweza. Kwa hiyo jamii isimsahau mtoto wa kike, impe fursa sawa na mtoto wa kiume,” Mwalimu Mwita amesisitiza.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Nyansincha, Edina Mwita Nyambacha ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuwapa watoto wa kike kipaumbele katika suala la elimu, ili waweze kufikia malengo yao.

“Wazazi nao watupatie fursa ya kupata elimu bora ili tuweze kufikia malengo yetu kama Rais Samia na pia tuweze kuwasaidia katika maisha ya baadaye,” ameongeza.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Mtoto wa Kike yamefanyika sambamba na mashindano mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi Nyansincha, Nyantira na Muringi, yakiwemo ya kucheza mpira, kuvuta kamba na kusoma.


Mashindano ya kuvuta kamba

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, yalianzishwa na Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kuendeleza harakati za kuhamasisha ustawi wa kijinsia kwa watoto wa kike na haki zao za msingi, ikiwemo ya kupata elimu bora.

Awali, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota amesema wanashirikiana na wadau mbalimbali kutekeleza shughuli za maendeleo ya jamii.

Miongoni mwao amesema ni Right to Play ambaye wanashirikiana naye kutekeleza mradi unaolenga kuongeza ubora wa elimu na elimu jumuishi katika kata ya Nyansincha.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages