NEWS

Wednesday 17 November 2021

Changamoto za hedhi kwa wasichana shuleni: NIMR yataja mwarubaini
TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema changamoto za hedhi kwa wanafunzi wa kike wa shule za msingi na sekondari, zinaweza kubaki historia nchini, ikiwa kwanza elimu na uhamasishaji endelevu kwa umma vitazingatiwa.

“Hatua hizo zitasaidia kuongeza uelewa na kujenga mtizamo chanya ili kuendana na afya na usafi wakati wa hedhi,” Mtafiti Mwandamizi wa Afya kutoka NIMR, Dkt Robert Njee amesema.


Dkt Robert Njee

Dkt Njee ameyasema hayo wilayani Rorya Novemba 16, 2021 wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti wa hedhi salama, uliofanywa na taasisi hiyo kati ya Februari na Septemba 2019, katika halmashauri 19 (ikiwemo Rorya) za mikoa 16 Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar).

Amesema elimu ni muhimu katika kuchochea ushiriki wa jamii, kuondoa miiko na kuwafanya watu wa jinsi zote kuiona hedhi ni kitu cha kawaida.

Kwa mujibu wa NIMR, vijana na wazazi wa kiume wanastahili kupewa elimu ya hedhi na kuhakikisha kunakuwepo walimu wa kike wa kutosha, ili kuchochea mienendo bora ya afya na usafi wakati wa hedhi.


Sehemu ya wajumbe wa kikao maalum cha kuwasilisha utafiti huo

“Kuna haja pia ya kuboresha elimu kazini kwa walimu wa kiume na wazazi kuhusu namna bora ya kuwasiliana na wasichana wakati wa hedhi, kwa sababu kukosekana kwa uelewa juu ya hedhi ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuchangia ushiriki duni wa wanaume katika masuala ya hedhi,” Dkt Njee ameongeza.

NIMR inapendekeza pia kwamba Serikali na wadau hawana budi kubuni na kutekeleza mbinu za kuzijengea shule za msingi na sekondari uwezo wa kuboresha miundombinu ya maji na vyumba maalumu kwa ajili ya kutumiwa na watoto wa kike kujisitiri wakati wa hedhi.

Pia, kuna haja ya kuwajengea walimu na wazazi uwezo ili kuwasaidia na kuwawezesha wasichana kuendelea na masomo wakati wa hedhi.“Aidha, kuna haja ya kuimarisha mfumo wa huduma ya hedhi shuleni, hususan kuhakikisha kunakuwepo dawa za kupunguza maumivu na msaada wa kisaikolojia kwa wasichana walio kwenye hedhi.

“Lakini pia, miongozo ya afya na usafi wakati wa hedhi na mtaala havina budi kupitiwa na kuweka uzito, hasa katika muktadha wa wanafunzi wenye ulemavu,” inaongeza sehemu ya mapendekezo ya NIMR.Awali, Dkt Njee ametaja sababu zilizotolewa wakati wa utafiti huo kuhusu wasichana kutohudhuria shule kipindi cha hedhi, kuwa ni pamoja na maumivu na usumbufu, kukosa vifaa vya hedhi, hofu ya kudhalilika endapo nguo zitachafuka damu, ukosefu wa vyumba vya kubadilishia nguo na huduma bora za vyoo na maji.

Akichangia hoja katika kikao cha kuwasilisha matokeo ya utafiti huo, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Lucy Mtesigwa amesema kuna haja ya maofisa elimu kuhakikisha kila shule inakuwa na walimu wa kike ili pia waweze kusaidia wanafunzi wa kike wakati wa hedhi.


Lucy Mtesigwa

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka yeye amesema matokeo ya utafiti huo uliofanywa na NIMR huenda yakawa chachu ya suluhisho la changamoto za hedhi zinazowakabili wasichana shuleni.

“Baada ya utafiti ni vizuri sasa tuelekee kwenye kutengeneza sera itakayotatua changamoto hizo za hedhi kwa watoto wetu wa kike. Hedhi ni jambo la kibaiolojia, siyo laana, hivyo tusiruhusu imani, mila na desturi ambazo hazifai kukwaza juhudi za kuwaondolea mabinti matatizo hayo,” Chikoka amesema.


Juma Chikoka

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Francis Namaumbo amesema matokeo ya utafiti huo yatachochea nguvu ya kuweka na kutetea bajeti ya kukabiliana na changamoto za hedhi kwa watoto wa kike.

“Katika kipindi hiki cha uandaaji wa bajeti na mipango ya maendeleo, tunakwenda kulitazama suala hili kwa kina na kuweka bajeti itakayosaidia kupata taulo za kike, lakini pia kuwashirikisha wadau ili kuweka mazingira ya upatikanaji wa vifaa hivyo,” Namaumbo amesema.

Namaumbo akizungumza kikaoni

Naye Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Shirika la Maji Safi Group lililopo Shirati wilayani Rorya, Rahel Steven amesema nao wamejikita katika kutoa elimu ya hedhi salama kwa watoto wa kike.


Rahel Steven

“Tumejikita katika kuvunja ukimya kuhusu masuala ya hedhi, kuelekeza jamii na watoto wa kike namna nzuri ya kujisitiri ikiwemo upatikanaji wa vifaa bora vya kujisitiri, sehemu yenye usiri kwa ajili ya kujisitiri, utupaji na uhifadhi wa vifaa vya hedhi baada ya kutumika,” Rahel amesema.
 
Makala maalum kuhusu matokeo ya utafiti huo uliofanywa na NIMR itachapishwa kwenye gazeti la Sauti ya Mara Jumatatu ijayo.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages