NEWS

Friday, 12 November 2021

Kikao cha wadau wa maji Tarime: Watendaji wa vijiji, kata wahimizwa kusimamia utunzaji miundombinu




MAOFISA watendaji wa vijiji na kata wilayani Tarime, Mara wamehimizwa kusimamia ulinzi na utunzaji wa miundombinu ya miradi ya maji, ili kuimarisha huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo yao ya uongozi.

Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime, Mhandisi Malando Masheku amesisitiza hayo wakati wa kikao cha wadau wa maji kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kilichofanyika ukumbi wa TTC, leo Novemba 12, 2021.


Mhandisi Masheku (kulia) akizungumza kikaoni

Pia Mhandisi Masheku amewakumbusha watendaji hao jukumu la kushiriki vikao vya jumuia za watumia maji katika maeneo yao ya uongozi, ili kujua changamoto zinazokabili miradi ya maji na kusaidiana kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa mujibu wa meneja huyo, upatikanaji wa maji kupitia miundombinu ya bomba na visima katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa sasa ni asilimia 70.


Wajumbe kikaoni

“Tuna miundombinu 14 inayofanya kazi na visima vya pampu za mkono 584. Tunazalisha lita milioni sita kwa siku na mahitaji ni lita milioni 11.9,” Mhandisi Masheku amefafanua.

Aidha, meneja huyo wa RUWASA amesema ofisi yake imefanikiwa kuhuisha miradi miwili kati ya mitatu ‘kichefuchefu’ iliyokuwa imesimama kufanya kazi kwa miaka 12.

Ametaja miradi hiyo ya maji kuwa ni Gibaso na Magoto, huku kwa sasa wakiendelea na utekelezaji wa mradi wa Sirari.


Sehemu nyingine ya wajumbe kikaoni

“Tunaendelea kutekeleza mradi wa Sirari, tunaamini kufikia Desemba 30, 2021 wananchi watakuwa wameanza kupata maji safi na salama kutokana na chemchem ya kisima cha asili, utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha lita 15,000 kwa saa,” Mhandisi Masheku amesema.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa amewataka maofisa watendaji wa vijiji na kata kusaidia kuelimisha wananchi umuhimu wa vyanzo vya maji na miundombinu yake, ili washiriki kikamilifu kuilinda na kuitunza.


Marwa akizungumza kikaoni

Marwa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Wilaya, Col. Michael Mntenjele kama mwenyekiti wa kikao hicho, ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kufichua waharibifu wa miundombinu ya maji ili wachukuliwe hatua za kisheria.

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages