NEWS

Saturday 13 November 2021

Balozi wa Ujerumani, mamia ya wanariadha washiriki mbio za Serengeti Safari Marathon 2021




BALOZI wa Ujerumani nchini Tanzania, Regine Hess, leo Novemba 13, 2021 ameungana na mamia ya wanariadha kushiriki mbio za Serengeti Safari Marathon 2021 katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Napenda kuja Serengeti kushiriki mashindano haya na wengine na katika maeneo mazuri (interesting places) kama Serengeti,” Balozi Hess ameiambia Mara Online News, mara baada ya kukimbia kilometa tano katika mbio hizo zilizovutia mamia ya washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Balozi Hess (kulia) akishiriki mbio hizo

Balozi Hess amesema amefurahi kushiriki mbio hizo kwani Serikali ya Ujerumani hutumia kiasi kikubwa cha fedha kusaidia uhifadhi katika ikolojia ya Serengeti kupitia Shirika la Kimataifa la UHifadhi la Frankfurt Zoological Society (FZS) lenye makao makuu nchini Ujerumani.

Pia, Balozi Hess ameeleza kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kudumisha uhifadhi na kukabiliana na vitendo vya ujangili.
Balozi Hess akivishwa medali mara baada ya kuhitimisha mbio zake.

Katika hatua nyingine, Balozi huyo wa Ujerumani ameeleza kufurahishwa na ongezeko la idadi ya watalii wanotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitatu mfululizo.

“Utalii uliathirika kutokana na tatizo la UVIKO-19, lakini tunafurahi idadi ya watalii imeanza kupanda sasa,” amesema.

Wafanyakazi wa FZS Serengeti wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo za Serengeti Safari Marathon 2021, zilizohusisha kilomita 42, 21, 10 na 5.
MasegeriBalozi Hess katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa FZS Serengeti, baada ya kuhitimisha mbio hizo.

“Sisi kama shirika la uhifadhi tunaunga mkono juhudu za utalii wa ndani, maana ni sehemu ya kuingiza kipato kwa ajili ya kusadia uhifadhi, kwani uhifahi unahitaji fedha nyingi,” Meneja Miradi wa FZS Serengeti, Masegeri Rurai amesema.

Rurai amesema mbio hizo pia zimeshuhudia ushiriki kutoka Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW), ambayo pia ni mdau wa uhifadhi katika ikolojia ya Serengeti.

Masegeri Rurai (kushoto) akishiriki mbio hizo

“Haya mashindano ni muhimu, yanatangaza utalii na kuhamasisha uhifadhi na yanafanyika wakati mwafaka wa migration ya nyumbu (uhamaji wa wanyamapori aina ya nyumbu),” Rurai ameongeza.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Masana Mwishawa amesema mbio za Serengeti Safari Marathon 2021 zimekuwa na mafaniko makubwa, kwani yamekuwa na washiriki wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Mhifadhi Mwishawa (kushoto) akiteta jambo na Balozi Hess baada ya wote kushiriki mbio hizo.

“Mashindano ya mwaka huu yamefana sana, tumeona wageni kutoka nje ni wengi, mwaka jana washiriki kutoka nje hawakuwa wengi kutokana na janga la korona [KOVID-19], lakini mwaka huu washiriki kutoka Ulaya na Kenya ni wengi.

“Watazania wengi pia wamejitokea kutoka mikoa mbalimbali na wenyeji kutoka wilaya za mkoa wa Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na tumefurahi pia kuona washiriki kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro,” Mwishawa amesema.

Ameongeza “Kwa kweli hamasa ni kubwa na kuna sababu, tumekuwa wabuni zaidi kwa kushirikiana na waandaaji… mafunzo mbalimbali yametolewa kwa wadau, yakiwemo ya ujasiriamali. Tunataka mashindano haya yawe chachu ya kukuza uchumi wa wananchi, siyo kuiingizia Serikali kipato tu, tunaangalia na wananchi wanaishi jirani na Hifadhi ya Serengeti.”



Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameshiriki pia katika mbio hizo, kisha kukabidhi zawadi mbalimbali zikiwemo za fedha taslimu kwa washindi.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages