NEWS

Wednesday 10 November 2021

RC akagua ujenzi wa vyumba vya madarasa Tarime Mji, ataka kasi iongezwe




MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Ally Hapi amekagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime na kutaka kasi iongezwe, ili ukamilike kwa wakati kwa ajili ya kuwaondolea wanafunzi mirundikano madarasani.

“Ongezeni kasi, fedha zote zimeshaletwa, Rais Samia Suluhu Hassan anataka watoto wasome wakajenge Taifa. Ukimpa mtoto wa maskini elimu unakuwa umemkomboa,” RC Hapi amesema.


RC Hapi (kulia) akitoa maelekezo wakati wa ukaguzi wa ujenzi huo

Amesisitiza hayo leo Novemba 10, 2021 wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Mogabiri na vingine viwili vya shule shikizi ya Gederi, nje kidogo ya mji wa Tarime.



Mkuu huyo wa mkoa ametumia nafasi hiyo pia kuwaomba viongozi na wananchi wa halmashauri hiyo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia katika kuwaletea Watanzania maendeleo ya kisekta, huku akionya ubadhirifu dhidi ya fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa.

“Mtu yeyote asithubutu kutengeneza utaratibu wa tumbo lake kwenye fedha hizi,” ameonya.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye maarufu kwa jina la Namba Tatu, amewaomba watekelezaji wa miradi hiyo ya elimu kuwatumia vijana wa maeneo husika ili kuwongezea kipato.


Namba Tatu (mwenye kipaza sauti) akizungumza katika ziara hiyo

Nao Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote na Diwani wa Kata ya Ketare, Daudi Wangwe wamemshukuru Rais Samia kupitia kwa RC Hapi na kuahidi kufuatilia na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.

Hivi karibuni, Serikali chini ya Rais Samia imeipatia Halmashauri ya Mji wa Tarime mamilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi ya 30, vikiwemo vya shule za sekondari na shule shikizi.

Fedha hizo ni sehemu ya Sh trilioni 1.3 ambazo Serikali chini ya Rais Samia imepewa mkopo kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa ajili ya kugharimia Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, yenye kaulimbiu inayosema “Pambana na UVIKO-19, Kazi Iendelee”.

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages