NEWS

Thursday 9 December 2021

CCM Tarime wamuaga Katibu Mkaruka aliyehamishiwa Butiama kwa kishindo



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, kimemuaga rasmi aliyekuwa Katibu wa Wilaya hiyo, Hamis Mkaruka, katika sherehe iliyofana kwa aina yake.

Katibu Mkaruka alihamishiwa wilaya ya Butiama mkoani Mara hivi karubuni na nafasi yake kuchukuliwa na Valentine Maganga.



Sherehe ya kumuaga Mkaruka imefanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya CMG mjini Tarime leo Desemba 9, 2021, ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho tawala wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Mntenjele.

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simon K. Samwel, wenyeviti wastaafu wa CCM Wilaya ya Tarime, Simon Wangwe na Rashid Bogomba, miongoni mwa wengine.



Sherehe hizo zimehusisha matukio ya kula, kunywa, kucheza muziki na kumkabidhi Katibu Mkaruka zawadi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na cheti maalum cha heshima, kitambaa cha suti na fedha taslimu.


Mwenyekiti Ngicho (wa pili kulia) na Mwenyekiti Simon K. Samweli (kushoto) wakimkabidhi Mkaruka cheti maalum cha heshima. Kulia ni Katibu Maganga.


Mkaruka (kulia) akifurahia zawadi ya kitambaa cha suti


Ufunguzi wa shampeni ukumbini



Akizungumza katika sherehe hizo kwa niaba ya wana-CCM Tarime, Mwenyekiti Ngicho amesema Mkaruka anastahili kupongezwa, kwani utumishi wake ulichangia kukipatia chama hicho ushindi wa kishindo katika majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Ngicho ametumia nafasi hiyo pia kuwataka viongozi wa CCM, madiwani na wanachama wa chama hicho kumpa ushirikiano Katibu mpya, Maganga na watumishi wa Serikali, ili kuharakisha maendeleo ya wananchi katika halmashauri za Tarime Mji na Tarime Vijijini.


Mwenyekiti Ngicho akizungumza

“Madiwani endelezeni umoja na mshikamano wenu, umoja wenu ndiyo mafanikio yenu. Epukeni majungu, jukumu lenu kubwa liwe kuchapa kazi na kushughulikia maendeleo ya kata zenu, ikiwemno kusimamia ujenzi wa vyumva vya madarasa,” Ngicho amewahimiza madiwani wa halmashauri hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), K Samwel ameahidi kuendeleza utumishi uliotukuka kwa CCM na wananchi kwa ujumla, ili kulinda heshima ya chama hicho tawala, ikiwa ni pamoja na kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.


Mwenyekiti K. Samwel akizungumza

Alipopewa nafasi, Katibu Mkaruka mbali na kuwashukuru wana-CCM Tarime kwa sherehe hiyo, amempongeza Mwenyekiti Ngicho, akisema ndiye anastahili kubeba kwa sehemu kubwa heshima ya kurejesha majimbo ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini kwenye himaya ya chama hicho.


Katibu Mkaruka akizungumza

Naye Katibu mpya wa Wilaya ya Tarime, Maganga ameahidi kuendeleza mazuri yaliyoachwa na Katibu Mkaruka, ikiwa ni pamoja na kushirikiana na viongozi wengine kutatua kero za wananchi katika wilaya hiyo.



(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages