NEWS

Monday, 20 December 2021

Mabinti waliokimbilia Shirika la Hope for Girls kukwepa ukatili wahitimu mafunzo ya ushonaji, ujasiriamali




MABINTI 12 (pichani juu) waliokimbilia Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) kukwepa ukatili wa kijinsia katika familia zao, wamehitimu mafunzo ya ushonaji na ujasiriamali.

Mahafali yao yamefanyika Desemba 18, 2021 katika kituo cha HGWT, nje kitogo ya mji wa Mugumu, Serengeti mkoani Mara, ambapo mabinti hao kila mmoja amepewa cherehani.


Wakikabidhiwa vyerehani

Kupitia risala yao kwa mgeni rasmi, mabinti hao wamesema wamejifunza kushona nguo, vikapu, mikoba na kutengeneza sabuni za maji, miongoni mwa fani nyingine.


Wakisoma risala


Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji akimkabidhi mmoja wa mabinti hao cheti cha kuhitimu mafunzo hayo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa HGWT, Rhobi Samwelly, mabiti hao wamepata mafunzo hayo kwa miaka mitatu katika nyumba salama za shirika hilo; moja ikiwa Mugumu, Serengeti na nyingine wilayani Butiama.

Rhobi amesema katika kipindi cha mwaka 2021, shirika hilo limeweza kutoa huduma mbalimbali kwa watoto 171, wengi wao wakiwa wahanga wa ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na ubakaji.

“Ushauri wa kisaikolojia umetolewa kwa wahanga 171 kutoka wilaya za Serengeti, Butiama, Tarime na Rorya na kuwawezesha kuishi kwa amani na kuwa tayari kuwaeleza maofisa ustawi wa jamii na mahakama ukatili waliofanyiwa.

“Aidha, wahanga wanaopata hifadhi kwenye vituo vyetu hupata huduma za chakula, malazi, matibabu, mavazi na kuendelezwa kielimu katika shule za msingi, sekondari na vyuo,” Rhobi ameongeza.


Rhobi akisoma taarifa fupi ya HGWT

Mkurugenzi huyo amesema Shirika la HGWT kwa kushirikiana na ofisi ya ustawi wa jamii na dawati la jinsia la wanawake na watoto ndani ya Jeshi la Polisi, wameweza kufikia watu 100,651 katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, kuwaelimisha madhara ya ukatili wa kijinsia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Serengeti, Dkt Vicent Mashinji aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, amewataka mabinti waliohitimu mafunzo hayo kuwa mabalozi wema wa kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni katika jamii.


DC Mashinji akihutubia

“Takwimu zinaonesha ukatili uko juu wilayani Serengeti, sisi kama Serikali hatutaruhusu mambo haya kuendelea,” DC Mashinji amesema na kuahidi kusaidiana na Shirika la HGWT kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazolikabili, ikiwemo kupata eneo kubwa kwa ajili ya shughuli za kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia.

(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages