NEWS

Sunday 19 December 2021

Musoma Vijijini wachangamkia ujenzi wa 'high schools' za masomo ya sayansi



Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo

WANANCHI wa Musoma Vijijini wameanza kuchangamkia ujenzi wa shule za sekondari za juu za masomo ya sayansi, ili kuinua ufaulu kwa wanafunzi na kupunguzia wazazi mzigo wa kusafirisha watoto wao kwenda kusoma nje ya jimbo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini kwa vyombo vya habari jana, juhudi kubwa zimeelekezwa kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa na maabara.

Miongoni mwa shule zilizojipanga kuwa na kidato cha tano hadi cha sita kwa masomo ya sayansi ni Shule ya Sekondari ya Bugwema.

Tayari shule hiyo imekamilisha ujenzi wa maabara tatu za masomo ya Baiolojia, Fizikia na Kemia kutokana na fedha zilizotolewa na Serikali, Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo na wadau wengine wa maendeleo.

Lakini pia ilishajenga vyumba viwili vya madarasa, na hivi karibuni Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeipatia fedha za kugharimia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu.

“Hakika wananchi tunafurahi na tunawashukuru viongozi wetu, hasa Rais Samia na Mbunge Profesa Muhongo kwa kutupunguzia mzigo wa elimu kwa watoto wetu,” Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Masinono, Morice Wasige amesema.


Mwenyekiti Morice Wasige

Hata hivyo, shule hiyo ina hitaji la mabweni ya wanafunzi, changamoto ambayo wananchi wa kata ya Bugwema wanasema sasa ni jukumu lao kuhakikisha inapata ufumbuzi.

“Tukipata mabweni katika shule hii ufaulu utaongezeka, maana umeme upo na maabara zipo - zitawezesha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo, japokuwa pia kuna hitaji jingine la maji,” Wasige amesema.

(Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages