TAASISI ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania (MISA-TAN), imekutanisha wamiliki wa vyombo vya habari nchini kujadili nafasi ya vyombo vya habari na uhuru wa kiuhariri kwa maslahi ya umma.
Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyoshiriki mkutano huo jijini Dodoma leo Desemba 15, 2021, ni Gazeti la Sauti ya Mara likiwakilishwa na Christopher Gamaina ambaye pia ni Mhariri Mkuu wa gazeti hilo.
Akiwasilisha mada, Mhariri Mwandamizi na Mshauri wa Vyombo vya Habari nchini, Jesse Kwayu amesema wamiliki wana nafasi kubwa ya kusaidia vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru, uwazi na haki, badala ya kuingilia na kudidimiza dhana hizo.
“Uwazi una thamani kubwa kwa umma, ni ishara ya utawala bora, unawezesha jamii kuwa huru kila kitu,” Kwayu amesema.
Kwayu akiwasilisha mada
Naye Mwandishi wa Habari Mwandamizi nchini, Jenerali Ulimwengu katika mada yake, amesisitiza kuwa utawala wowote unaokandamiza uhuru wa vyombo vya habari unatoa mwanya wa maovu, ikiwemo rushwa na wizi wa mali za umma.
“Bila vyombo vya habari vyenye nguvu ya uhuru, ni sawa na kuwa na miundombinu bila wahandisi,” amesema Ulimwengu na kuongeza kuwa uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari utakuwa na tija kwa umma.
Jenerali Ulimwengu (kulia) akiwasilisha mada
Katika majadiliano hayo, washiriki wamelalamikia vitisho vya hatari vinavyotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali na wa kisiasa, hasa wa chama tawala kwa waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari, kwamba vinachangia kuua uhuru na uwazi wa habari zenye tija kwa umma nchini.
Awali, Afisa Habari na Msimamizi wa Mradi wa MISA TAN, Jacqueline Jones amesema majadiliano hayo yanalenga kuimarisha uhuru wa habari nchini na kwamba taasisi hiyo inashirikiana na International Media Support (IMS) katika juhudi hizo, kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).
Jacqueline akizungumza mkutanoni
(Imeandikwa na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment