NEWS

Friday 21 January 2022

Chege agawa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi Rorya




MBUNGE wa Rorya mkoani Mara, Jafari Chege (pichani juu), leo Januari 21, 2022 amegawa msaada wa sare za shule kwa wanafunzi 31 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

Mbunge Chege amewakilishwa na wasaidizi wake kugawa msaada huo katika Shule ya Msingi Erengo walikosoma wanafunzi hao.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Marwa Matatiro amesema kati ya wanafunzi 31 waliopata msaada huo wa sare za shule, 16 ni wasichana na wavulama 15.

 Wasaidizi wa Mbunge Chege wakigawa sare za shule kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza

Msaada huo ni utekelezaji wa ahadi ya Mbunge Chege aliyotoa kabla ya wanafunzi kufanya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Darasa la Saba mwaka jana.

Akizungumza na Mara Online News kwa njia ya simu leo, Mbunge Chege amesema hadi sasa anawezesha wanafunzi 128 kupata elimu ya msingi, sekondari na chuo kwa kuwanunulia sare na kuwalipia ada za shule.

“Hawa wanafunzi wako katika maeneo tofauti tofauti ndani ya jimbo, lakini nimejitahidi kuzingatia kila kata ninakuwa na wanafunzi wa kusaidia,” Mbunge Chege amesema.

Amefafanua “Ninawasaidia ada, hasa wanaoenda vyuo vya ufundi kwa maana ya VETA, na kuna ambao nawasaidia kwenda advance [akimaanisha kidato cha tano na sita].

“Lakini pia kwa darasa la kwanza mpaka la saba na form one (kidato cha kwanza) mpaka form four (kidato cha nne) kwa sababu hakuna ada, hawa nawasaidia uniforms (sare).”

 Wazazi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliopata msaada wa sare za shule 

Mbunge huyo amesema amejiwekea utaratibu wa kuhakikisha kuwa kila mwaka anasaidia watoto wa familia zisizojiweza kiuchumi katika jimbo la Rorya kupata elimu.

“Na leo tumekabidhi uniforms pale Erengo shule ya msingi, hawa ni watoto waliofaulu kwenda form one lakini wazazi wao wamekosa uwezo wa kuwapatia uniforms, na maeneo mengine tunaendelea na utaratibu huo huo,” amesema.

Chege ameongeza kuwa wiki ijayo ataendelea kugawa sare za shule kwa wanafunzi wote wenye uhitaji huo. “Lakini pia kwa upande wa ada napo tunafanya hivyo hivyo ndani ya jimbo,” amesema.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages