NEWS

Friday 21 January 2022

Tarime Mji wakamilisha ujenzi wa madarasa 32, wayakabidhi kwa RC Mara


HALMASHAURI ya Mji wa Tarime imekabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi vyumba vipya vya madarasa 32 ya shule za sekondari na shikizi.

Makabidhiano hayo yamefanyika juzi, baada ya RC Hapi kukagua baadhi ya madarasa hayo, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika Shule ya Sekondari ya Turwa.

Ujenzi wa madarasa yote 32 umegharimu shilingi milioni 640 ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya kampeni ya maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

RC Hapi ameipongeza halmashauri hiyo kwa kukamilisha ujenzi huo kwa asilimia 100 na kuwezesha mamia ya wanafunzi kusoma bila msongamano.


RC Hapi (wa pili kushoto) akielezea kuridhishwa na ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa katika sekondari ya Nkende

“Hongereni sana kwa majengo mazuri na matumizi mazuri ya hizo pesa,” amesema na kuongeza kuwa ujenzi wa madarasa hayo ni zao la ubunifu wa Rais Samia.

“Isingekuwa madarasa haya, hata walimu wanajua, tulikuwa tunaulizana hapa watoto wa kidato cha kwanza wataingia wapi. Kuna sehemu nimekuta shule ilikuwa na upungufu wa madarasa sita, sasa sijui hata wazazi wangekamuanaje kujenga madarasa sita,” RC Hapi amesema.


RC Hapi akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza katika sekondari ya Nkende

Miongoni mwa viongozi wengine walioshiriki katika makabidhiano hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo, ambao wamewataka walimu na wanafunzi kutunza madarasa hayo yadumu muda mrefu.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amekemea wakuu wa shule wanaoanzisha michango isiyo rasmi na kusababisha wanafunzi wengi kufukuzwa shule na kupitwa na masomo.


RC Hapi akihutubia mkutano wa hadhara katika sekondari ya Turwa

“Kauli ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kwamba mwanafunzi yeyote asizuiliwe kuingia darasani kwa sababu ya michango na asihusishwe kwa namna yeyote. Kama itakuwepo ambayo imepitishwa na serikali basi ahusishwe mzazi moja kwa moja,” amesisitiza.

Kwa upande mwingine, serikali imetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la OPD katika zahanati ya Magena na shilingi milioni 150 kugharimia ujenzi wa maboma katika zahanati tatu ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tarime.

Pia, serikali imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa chumba maalumu cha wagonjwa wa dharura katika hospitali ya halmashauri hiyo.

“Nataka niwahakikishie wana-Tarime kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan yupo kazini na anachapa kazi, yote haya mnayoyaona ameyafanya ndani ya miezi tisa tu ya uongozi wake, hivyo ni lazima tumuunge mkono,” RC Hapi amesema kwenye mkutano wa hadhara.

(Habari na picha zote: Geofrey John)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages