NEWS

Friday 21 January 2022

CCM yamteua Dkt Tulia kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania



ALIYEKUWA Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Tulia Ackson Mwansasu (pichani juu), ameteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kugombea nafasi ya Spika wa Bunge hilo.

Hayo yameelezwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, baada ya kumalizika kwa kikao maalumu kilichoongozwa na Mwenyekiti wake, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi ya Spika wa Bunge ulifanyika kati ya Januari 10 na 15, 2022 baada ya Job Ndugai kujiuzulu wadhifa huo Januari 6, mwaka huu ambapo wanachama 71 wa CCM walijitokeza kuchukua na kurejesha fomu hizo.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia kwa utendaji wake mzuri wa kazi, ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu wanaanza masomo kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa nchini.

Pia, imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt Hussein Ali Mwinyi, kutokana na utendaji wake mzuri, ikiwemo kusimamia uchumi wa bluu.

#MaraOnlineNews-Updates

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages