NEWS

Monday 21 February 2022

Vigogo wengine NHIF wapandishwa kizimbani Musoma kwa uhujumu uchumi
IDADI ya vigogo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 23 ya mwaka 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma mkoani Mara, imefika 11 baada ya wengine wawili kupandishwa kizimbani.

Waliopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka jana mbele ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka ni wakaguzi wa ndani wa NHIF - Makao Makuu, Julius Mziray na Zakayo Mampagwa. Hawakutakiwa kujibu lolote, kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Awali, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Nimrod Byamungu aliieleza Mahaka hiyo kuwa Mshtakiwa wa 10, Mziray katika hati ya mashtaka yenye makosa 30, anakabiliwa na makosa mawili (la kwanza na la 30), kama ilivyo kwa mshitakiwa wa 11, Mampagwa.

Wakili Byamungu aliieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao kwa kushirikiana na wenzao tisa wakiwa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na mkoani Mara, kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2013 na Machi 2016, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia shilingi 3, 003,879,686 mali ya NHIF.

Alisema kosa la pili linalowakabili ni la 30 katika hati hiyo ya mashtaka, ambapo ilielezwa kuwa wote walimsababishia mwajiri wao [NHIF] hasara ya shilingi zaidi ya bilioni tatu.

Wakati upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na Wakili Byamungu akishirikiana na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), William Nyamboko, washtakiwa hao waliwakilishwa na mawakili watatu wa kujitegemea; Ostack Mligo, Thomas Msasa na Angero James.

Februari 14, mwaka huu, waliosomewa mashtaka mahakamani hapo na nyadhifa, vyeo na vituo vyao vya kazi vikiwa kwenye mabano ni mshtakiwa wa nne, Jesca Mataba (Mhasibu Msaidizi NHIF - Mara), mshtakiwa wa tano, Grace Godi (Mhasibu Mkuu NHIF -Dar es Salaam), mshtakiwa wa sita, Anne Maneno (Mkaguzi Mkuu wa Ndani NHIF - Dar es Salaama) na mshtakiwa wa saba, Myriam Fungameza (Afisa Madai HNHIF - Dar es Salaam).

Wengine waliosomewa mashtaka mahakamani hapo Februari 17, mwaka huu ni mshtakiwa wa nane, Goodluck Kirabe (Kaimu Mhasibu Mkuu NHIF - Dar es Salaam) na mshtakiwa wa tisa, Deusdedit Rutazaa (Mkurugenzi wa Uendeshaji na Uwekezaji NHIF - Dar es Salaam).

Washitakiwa wa kwanza kupandishwa mahakamani hapo Novemba 2, mwaka jana ni mshtakiwa wa kwanza, Francis Mchaki (aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa NHIF - Mara) anayeshtakiwa kwa makosa yote 30, wa pili ni Dkt Leonard Mitti (Msimamizi wa NHIF – Mara) na wa tatu ni Dkt Mgude Bachunya (Meneja wa NHIF - Mara.

Washtakiwa wawili waliofikishwa mahakamani jana waliungana na wenzao sita mahabusu, mpaka taratibu za kuwaombea dhamana zitakapokamilishwa katika Mahakama Kuu ya Kanda Musoma.

Kesi hiyo iliahirishwa mpaka leo mahakamani hapo, ambapo kila mshtakiwa atasomewa maelezo ya awali ya makosa yake.

Hakimu Rujwahuka alikubali ombi la Jamhuri kwa kuandika hati ya wito ili leo uongozi wa Magereza uwapeleke mahakamani washtakiwa walio mahabusu.

(Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages