NEWS

Tuesday 19 April 2022

TAKUKURU Tarime yamfikisha kizimbani mtaalamu wa afya kwa uhujumu uchumi



TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Tarime mkoani Mara, leo imemfikisha mahakamani aliyekuwa Afisa Afya wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Simon Nyandwera, akikabiliwa na mashtaka matano yanayoangukia kwenye kundi la rushwa na uhujumu uchumi.

Mashtaka namba moja, mbili na tatu ni ya kughushi, namba nne ni la ufujaji na ubadhirifu na la mwisho ni la kuisababishia Serikali hasara ya shilingi milioni 4.125.

Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU na Wakili wa Serikali, Mwinyi Yahaya amesoma mashtaka hayo yanayomkabili Nyandwera, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Yohana Myombo.

Yahaya ameiambia mahakama kuwa Nyandwera alitenda makosa hayo Oktoba 17, 2014 kinyume na Kanuni ya Adhabu [Sura ya 16 mapitio ya 2002], Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [Sura ya 329 mapitio ya 2002] na Sheria ya Uhujumu Uchumi [Sura ya 200 mapitio ya 2019].

Hata hivyo, mshtakiwa huyo amekana mashtaka hayo na amepelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, hadi Mei 2, mwaka huu kesi hiyo namba 13/2022 itakapoanza kusikilizwa mahakamani hapo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages