NEWS

Tuesday 5 April 2022

Wakuu shule za sekondari wakutana Sekondari ya Wasichana Tarime kujadili masuala ya kitaalumaWAKUU wa shule za sekondari za Serikali na binafsi zaidi ya 230 mkoani Mara, wamekuta katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Tarime, kujadili mambo mbalimbali ya kitaaluma.

Kikao chao kimefanyika Ijumaa Aprili 1, 2022 kwenye ukumbi wa shule hiyo inayomilikiwa na taasisi ya Professor Mwera Foundation (PMF).

Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera ametumia fursa hiyo kuwaomba viongozi hao kusaidia kuhamasisha vijana wa kike na kiume, wakiwemo waliohitimu kidato cha nne, kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na taasisi hiyo.Fani zinazotolewa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime ni pamoja na ufundi umeme, magari, udereva, ushonaji na kompyuta.

Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, amesema Taasisi ya PMF pia imeidhinishwa na Serikali kuendesha programu ya mafunzo ya kitaaluma kwa wafanyakazi wa sekta za hoteli na utalii katika mikoa 10.

“Mikoa hiyo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvuma,” amesema Hezbon ambaye pia ni mmoja wa wanachama wa chama tawala - CCM waliotia nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Tarime Mjini kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.“Vijana waliopata daraja la nne na alama sifuri wana fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi ili wasijione wametengwa… kupitia vyuo vya ufundi wanaweza kupanda hadi chuo kikuu na hatimaye kuajiriwa, au kujiajiri kutokana na fani walizosoma,” Hezbon amesema.


Hezbon akizungumza katika kikao hicho

Aidha, Mkurugenzi Hezbon amesema Taasisi ya PMF pia imetoa ofa kwa walimu wa mkoani Mara kwenda kupata mafunzo ya fani yoyote wanayohitaji katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime bila malipo.

Awali, akifungua kikao hicho, Afisa Elimu Mkoa wa Mara, Mwalimu Benjamin Oganga ameishukuru Taasisi ya PMF na kuitaja kama mdau mkubwa wa elimu anayestahili kuungwa mkono na viongozi wa elimu na seikali kwa ujumla katika juhudi za kuhamasisha elimu na mifumo ya kitaaluma.


Mwalimu Oganga (aliyesimama) akizungumza kikaoni

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages