NEWS

Tuesday 24 May 2022

Bundi azidi kugubika Rorya, baadhi ya madiwani wapuuza ushauri wa Mwenyekiti CCM Mkoa wa Mara



LICHA ya kutakiwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye “Namba Tatu” kuzika tofauti na migogoro isiyo na tija kwa wananchi, baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wamedaiwa kuwasilisha kwa Mkurugenzi Mtendaji barua ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wao, Gerald Ng’ong’a.

Taarifa zilizotufikia kutoka wilayani Rorya, zinasema madiwnai hao wamewasilisha barua hiyo leo, ikiwa ni siku moja baada ya Namba Tatu kukutana nao kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa ya Mkoa mjini Musoma na kuwataka kumaliza tofauti zao ili wajikite katika kuhamasisha shughuli za maendeleo ya wananchi katika halmashauri hiyo.



Aidha, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alihutubia kikao cha madiwani wa halmashauri hiyo na kuwataka kuacha malumbano na mwenyekiti wao, badala yake washirikiane kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hapi alikwenda mbali zaidi kwa kuonya kuwa endapo madiwani hao wataendelea na malumbano ambayo pia yanaripotiwa kuchangia kukwamisha utekelezaji miradi ya maendeleo ya wananchi, atazishauri mamlaka za juu serikalini kuivunja Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi

Lakini pia, mvutano huo wa madiwani na mwenyekiti wao umeendelea kushika kasi kipindi hiki ambacho Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka anasisitiza maridhiano ya kisiasa ndani ya chama hicho tawala.

Akizungumza na Mara Online News kwa njia ya simu leo, Diwani wa Kata ya Mkoma, Ayoyi Sonde amekiri kuwa yeye ndiye ameshirikiana na Diwani wa Kata ya Ikoma, Laurent Adrian kupeleka kwa Mkurugenzi Mtendaji barua ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti Ng’ong’a, wanayemtuhumu kukiuka kanuni za uongozi, ikiwa ni pamoja na kuwashtaki baadhi ya madiwani katika Jeshi la Polisi.

Kwa upande wake, Ng’ong’a alikiambia kikao cha Kamati ya Siasa mjini Musoma jana kwamba alilazimika kupeleka taarifa Polisi baada ya kubaini njama za baadhi ya madiwani kutaka kumteka.

Inaelezwa kuwa katika kikao hicho kilishohudhuriwa pia na Katibu wa CCM Mkoa, Langaeli Akyoo na Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Rorya, Charles Ochele, Mwenyekiti Ng’ong’a aliombwa akakubalia kuondoa malalamiko hayo Polisi.

Alipoulizwa kwanini hawakuheshimu ushauri wa viongozi wa mkoa akiwemo Namba Tatu wa kuwataka kuzika malumbano na mwenyekiti wao, Diwani Ayoyi amesema kikao hicho hakikuwa cha kusuluhisha mgogoro wao na Ng’ong’a, bali kilikuwa cha kusikiliza hoja za malalamiko yao dhidi ya mwenyekiti huyo.

“Sisi tunaendelea na harakati zetu, tumeshawasilisha barua kwa Mkurugenzi, tunasubiri aitishe kikao,” amesema Ayoyi ambaye aliwahi kuwa mwanachama wa CHADEMA na ACT Wazalendo kabla ya kutimkia chama tawala - CCM.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages