SHIRIKA la ATFGM Masanga limekutana na wadau kutoka idara na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, kujadili namna ya kushirikiana katika kusaidia watoto wenye ulemavu kupata haki zao kuanzia ngazi ya familia.
Kikao chao cha siku mbili kilichoratibiwa na kufadhiliwa na shirika hilo, kimehitimishwa leo Mei 24, 2022 katika Hoteli ya KIFA mjini Tarime.
Akifungua kikao hicho jana, Meneja Miradi wa ATFGM Masanga, Valerian Mgani alisema ni sehemu ya mpango kazi wa shirika hilo wa kwenda kutambua watoto wenye ulemavu, aina ya ulemavu walionao na mahitaji yao katika jamii wilayani Tarime.
“Mradi huu unafadhiliwa na Terre des Hommes Netherlands, lengo kuu ni kuunganisha wadau kwa ajili ya kupaza sauti ya kutetea haki za watoto wenye ulemavu wilayani Tarime,” alisema Mgani.
Valerian Mgani akiwasilisha mada kikaoni
Washiriki wa kikao hicho wamejikita zaidi katika kujadili na kupeana uzoefu kuhusu watoto wenye ulemavu, visababishi vya ulemavu, haki na wajibu wao, lakini pia mtazamo wa jamii juu yao.
Karibu washiriki wote wamesema watu wengi katika jamii wanaamini kimakosa kwamba ulemavu ni mkosi na laana, ilihali ni dosari zinazosababishwa na mapungufu ya homoni, ajali, ugonjwa, ukatili wa vipigo, huduma mbovu za afya na matumizi ya dawa zisizo rafiki kwa afya.
Wamekubaliana kwamba watoto wenye ulemavu wanastahili haki za kuishi kwa uhuru, kupewa jina, kucheza, kupata chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, kulindwa na kushirikishwa katika maamuzi, miongoni mwa stahiki nyingine kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ya Mtoto Namba 21 ya Mwaka 2009.
Mwanasheria kutoka Shirika la ATFGM Masanga, Irene Assey amesema utekelezaji wa mpango wa kwenda kuwatambua watoto wenye ulemavu pia utahusisha kuishawishi jamii kutunga sheria ndodo ndogo za kutetea na kulinda haki zao.
Makala maalumu yenye michango ya kina kutoka kwa washiriki wa kikao hicho itachapishwa kwenye toleo lijalo la gazeti la Sauti ya Mara linalochapishwa kila Jumatatu.
(Habari na picha zote: Mara Online News)
No comments:
Post a Comment