NEWS

Friday 20 May 2022

Mahakama ya Wilaya ya Tarime yamhukumu mwalimu kwenda jela miaka mitatu kwa kughushi hundi za shuleMAHAKAMA ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imemhukumu aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwege wilayani Rorya, kwenda jela miaka mitatu, au kulipa faini ya shilingi milioni 12, baada ya kumtia hatiani kwa makosa sita ya kughushi hundi za shule.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 306/2020 leo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Veronica Selemani amesema upande wa Jamhuri umethibitisha mashtaka yote sita dhidi ya mshtakiwa huyo.

Mashtaka hayo ni ya kughushi hundi za shule na kujipatia shilingi 4,965,000 ambazo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Mwege.

Makosa hayo ni chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Mapitio ya Mwaka 2019.

Hakimu Veronica amemhukumu mwalimu huyo (pichani chini) kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitatu gerezani, au kulipa faini ya shilingi 2,000,000 kwa kila shtaka.Pia mahakama imemuamuru mshtakiwa huyo kulipa fedha za mradi wa maendeleo, yaani za ujenzi wa vyumba vya madarasa kiasi cha shilingi 4,965,000 kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)/ Mahakama, alizochukua na kuisababishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasara.

Kwamba fedha hizo zingetumika ipasavyo kwenye maendeleo, nchi ingepiga hatua kubwa ya kuboresha utoaji wa huduma ya elimu nchini.

Shauri hilo lilifunguliwa na kuendeshwa na Wakili wa Serikali, Mwinyi Yahaya.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages