NEWS

Monday 23 May 2022

Mwenyekiti Halmashauri Rorya ajibu hoja za madiwani dhidi yake, aanika makubwa kwenye Kamati ya Siasa, Namba Tatu ataka suluhu



MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Gerald Ng'ong'a (pichani juu wa kwanza kushoto), amejibu hoja za madiwani wanaomtuhumu kukiuka taratibu za kiuongozi, ikiwemo kuwashtaki katika Jeshi la Polisi kwamba wanakula njama za kumteka na kutishia kumuua.

Ng'ong'a ameyasema hayo kwenye kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa mjini Musoma jana, chini ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye - maarufu kwa jina la Namba Tatu.

Licha ya kukiri kufikisha masuala hayo kwenye vyombo vya dola, Ng'ong'a ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Rabuor, amekanusha kuwafungulia mashtaka madiwani hao, na ameafikiana na Kamati ya Siasa kuwa hataliendeleza.

"Nilichofanya ni kupeleka taarifa kwenye vyombo vya kichunguzi, kuomba uchunguzi wa kina ufanywe baada ya mimi kufuatilia baadhi ya mambo ambayo nimejiridhisha yanahatarisha usalama wa maisha yangu," amesema Ng'ong'a.



Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ameongeza kuwa baada ya jaribio la kumuondoa kwenye wadhifa huo, alianza uchunguzi binafsi kwa ajili ya kujihakikishia usalama wake.

Amesema katika uchunguzi huo, alibaini aina ya gari na kutaja namba zake za usajili (zinahifadhiwa) limekuwa likitumiwa na madiwani anaowahusisha na mbinu ovu dhidi yake katika safari zao, zikiwamo za vikao vya usiku vya kupanga mikakati mibaya dhidi yake.

Ng’ong’a amesema pia alibaini kuwa mmoja wa viongozi wa wilayani Rorya ni miongoni mwa watu wanaofadhili mipango hiyo kwa kuwapa fedha madiwani ili kuchochea mgogoro huo.

Mgogoro huo unadaiwa kuhusisha na masuala ya kisiasa, hususan uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Hata hivyo, Namba Tatu amemtaka Ng'ong'a kuondoa suala hilo Polisi na kuwataka madiwani hao kuondoa tofauti zao, kwa sababu zinatia doa Halmashauri ya Rorya, mkoa wa Mara na kuathiri ustawi wa chama hicho tawala.



Naye Katibu wa CCM wa Mkoa huo, Langaeli Akyoo amesema anawajibika kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba kikao hicho ni moja ya hatua za Chama kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha hayafanyiki maamuzi yasiyokuwa sahihi.

Akyoo amesema baada ya kusikiliza hoja za madiwani na majibu ya Ng'ong'a, Kamati hiyo itazifanyia kazi kabla haijatoa taarifa ya uamuzi wa Chama kwa madiwani hao.

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages