NEWS

Monday 9 May 2022

Miili ya watu wanne waliokufa maji Rorya yapatikana

Vijana waogeleaji wakiwa katika harakati za kutafuta watu waliozama mto Mori wilayani Rorya. (Picha na Thomas Nkaina)

WAOGELEAJI wamefanikiwa kupata miili ya watu wanne waliokufa maji baada ya mtumbwi uliokuwa umewabeba kupinduka katika mto Mori wilayani Rorya, Mara juzi.

“Hadi leo tumepata miili minne ya wanawake watatu na mtoto wa kiume, yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Rorya – Utegi,” Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Kowak, Charles Peter ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio jioni hii.

Peter amesema bado vijana waliojitolea kutafuta watu waliozama majini mara baada ya ajali hiyo kutokea, wanaendelea kutafuta mtoto wa kike ambaye hajapatikana.

Inaelezwa kuwa mtumbwi uliopinduka katika mto huo unaotiririsha maji kuingia Ziwa Victoria, ulikuwa umebaba waumini wa kanisa la Roho Msanda waliokuwa wakivuka kelekea ibadani.

Vijana zaidi ya 20 ambao ni wabobezi wa kuogelea kutoka kijiji cha Kowak ilipotokea ajali hiyo, walijitosa majini kufanya kila wanaloweza ili kuwakoa watu watano ambao walizama baada ya mtumbwi huo kupinduka.

Kwa mujibu wa VEO huyo, mtumbwi uliopinduka ulikuwa umebeba watu wanane, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, watatu waliokolewa mara baada ya ajali hiyo.

Jeshi la polisi na mamlaka wilayani Rorya zilithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Wilaya ya Rorya inaripotiwa kuwa na miundombinu isiyo salama kwa usafiri wa majini.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages