NEWS

Sunday 12 June 2022

Serikali, wanavijiji waendelea kushirikiana ujenzi wa vituo vya afya Musoma Vijijini


SERIKALI inaendelea kutoa mamilioni ya fedha kuchangia ujenzi wa vituo vipya vya Afya vya Kiriba, Makojo na Kisiwa cha Rukuba katika jimbo la Musoma Vijijini.

“Katika ujenzi huo, Serikali ilitoa shilingi milioni 250 kwa kila kituo kwa ajili ya kuanza ujenzi wake,” imeeleza sehemu ya taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini leo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imetoa tena shilingi milioni 250 kuendeleza ujenzi wa vituo hivyo vipya naa kwamba fedha hizo za awamu ya pili zitapelekwa kwenye kata husika siku chache zijazo.

“Mchango wa shilingi milioni 500 kwa kila kituo kipya kinachojengwa jimboni mwetu ni mchango mkubwa. Tunaishukuru sana Serikali yetu, na kipikee kabisa tunamshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha fedha za utekelezaji wa miradi hii na mingine zinapatakina, ahsante sana,” taarifa hiyo imesema.

Hadi sasa, jimbo la Musoma Vijijini lenye kata 21 zinazoundwa na vijiji 68, lina kata tatu zenye vituo vya afya vinavyofanya kazi; ambavyo ni Murangi, Mugango na Bugwema.
Ujenzi wa kituo cha afya cha kata ya Makojo unaendelea

Aidha, kuna zahanati 26 zinazotoa huduma za afya katika jimbo hilo, kati ya hizo, 22 ni za Serikali na 4 ni za binafsi.

Kwa sasa zahanati mpya15 zinajengwa kwa nguvu ya wanavijiji na baadhi zimepokea michango ya fedha kutoka serikalini.

“Tunaomba michango na nguvukazi za wanavijiji iendelee kutolewa hadi kukamilika kwa ujenzi wa vituo vipya vya afya na zahanati zinazojengwa,” amesema Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo katika taarifa hiyo.

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages