WAKAZI wa kijiji cha Oliyo katika kata ya Rabour, wilaya ya Rorya mkoani Mara, wameutaka umma kupuuza upotoshaji unaoenezwa na watu wachache wenye nia mbaya kwamba hawatashiriki sensa ya watu na makazi Agosti 23, mwaka huu.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Gerald Ng’ong’a (kulia pichani juu) kijijini Oliyo wiki iliyopita, wananchi hao wamesema wako tayari kuhesabiwa wakati wa sensa hiyo.
“Wananchi wa kijiji cha Oliyo tuko tayari kushiriki sensa, tuko tayari kuhesabiwa kwa ajili ya maendeleo yetu na taifa letu, hayo yanayosemwa kwamba tutagomea sensa yapuuzwe maana ni shinikizo la watu wachache wenye nia mbaya,” amesema Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Marwa Mkwena.
Mwanakijiji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Magreth Fabian amesema “Sisi wana-Oliyo tuko tayari kuhesabiwa hata leo, maana suala la sensa ni la kitaifa, hivyo tunasubiri siku ifike ili wote tujitokeze kuhesabiwa.”
Kuhusu mradi wa ujenzi wa kituo cha afya unaoendelea katika kijiji cha Makongro katani hapo, wananchi hao wamesema wanauunga mkono kwani ukikamilika utakuwa msaada kwa wakazi wote wa kata hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri, Ng’ong’a ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Rabuor, amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo sensa ya watu na makazi.
“Sensa ni kwa faida na maendeleo yetu, twendeni tukahesabiwe tarehe 23 mwezi wa nane (Agosti) mwaka huu,” Ng’ong’a amewahamasisha.
Aidha, katika kuonesha umuhimu wa sensa ya watu na makazi, Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ameuliza ili kujua idadi ya akina mama waliokuwa na watoto mgongoni kwenye mkutano huo, kisha akagawa msaada wa miavuli 20.
“Nimeuliza mmesema akina mama wenye watoto katika mkutano huu ni 20, sasa nina jambo lao. Nimefanya hivi kama mfano wa maana ya sensa, kwamba lazima ujue idadi ya watu ili uweze kutenga bajeti itakayokidhi mahitaji yao,” amesema Ng’ong’a.
Ng'ong'a akizungumza katika mkutano huo
Mkutano huo umelenga kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa wananchi wa kijijini Oliyo, baada ya kuwepo uvumi kwamba watagomea sensa ya watu na makazi hadi ujenzi wa kituo cha afya Makongro utakapohamishiwa kijijini kwao.
Hivi karibuni, Serikali mkoani Mara imeutaka umma wa wananchi kupuuza upotoshaji unaoenezwa na watu wachache, kuhusu utaratibu wa kupata eneo la ujenzi wa kituo cha afya hicho.
Taarifa kwa umma, iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imesema uamuzi wa kujenga kituo hicho ulifikiwa na mamlaka husika, kwa kuzingati vigezo na taratibu za kisheria.
Taarifa hiyo imetaja vigezo vilivyozingatiwa kuwa ni pamoja na kupatikana kwa eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 10 unotosha majengo 12 yanayohitajika, ambalo limetolewa kwa hiari na wamiliki kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Pia, imesema eneo hilo limepitishwa na wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ya Rabuor kupitia vikao halali vya kisheria, lipo katika jiografia rafiki na linafikika kwa urahisi.
“Ujenzi wa kituo umeshanza na umefikia hatua ya lenta. Kituo hiki kikikamilika kitatumiwa na wananchi wa tarafa nzima ya Luo-imbo kama rufaa ya zahanati zilizopo.
“Aidha, katika kijiji jirani cha Oliyo, Serikali Kuu imepeleka shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha zahanati.
“Ndugu wananchi, uongozi wa Mkoa unawaomba kupuuza upotoshaji wowote kuhusu ujenzi wa kituo hiki cha afya. Mkoa utaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Stephano Amoni.
(Habari na picha: Sauti ya Mara Digital)
No comments:
Post a Comment