NEWS

Monday 18 July 2022

LVBC: Maandalizi ya 11 Siku ya Mara yameanza



MAANDALIZI ya Maadhimisho ya 11 ya Siku ya Mara (Mara Day) yameanza, kwa mujibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) inayoyaratibu.

“Ndiyo, maandalizi ya 11 ya Siku ya Mara yameshaanza na mwaka huu sherehe zake zitafanyika katika Jamhuri ya Kenya,” amesema Dkt Willy Mgenzi ambaye ni Afisa Mawasiliano na Uhamasishaji wa Maendeleo wa LVBC katika ujumbe wake mfupi kwa Sauti ya Mara Digital, hivi karibini.

Hata hivyo, Dkt Mgenzi amesema mataifa ya Kenya na Tanzania yatajadiliana kwa undani zaidi kuhusu namna gani sherehe hizo zitafanyika.

Nchi za Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha Siku ya Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara.

Lakini kwa miaka ya hivi karibuni, kila nchi imekuwa ikiadhimisha siku hiyo bila kukutana pamoja kutokana na tatizo la ugonjwa wa Corona.

Huenda tishio la Corona kwenye uendelevu wa maadhimisho hayo likafikia mwisho mwaka huu.

Kila maadhimisho hubeba kaulimbiu inayolenga kuhamasisha uhifadhi endelevu wa Mto Mara unaotiririsha maji ndani ya Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

Kwa kutambua umuhimu wa ikolojia ya Mara, kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda Mei 4, 2012 kiliazimia Septemba 15 kila mwaka kuwa Siku ya Mara.

Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mara yalifanyika mwaka 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalifanyika mwaka 2013 mjini Mugumu.

Kikundi cha ngoma ya asili kikitumbuiza wakati wa maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mara mjini Mugumu, Tanzania.

Maadhimisho hayo pia hutumika kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili ya Afrika Mashariki.

Mbali na kuchangia uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara katika nchi za Tanzania na Kenya.

(Imeandikwa na Sauti ya Mara Digital)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages