NEWS

Monday 1 August 2022

Rais Samia aapisha Wakuu wa Mikoa wapya, awaagiza mambo makuu mawili



Rais Samia Suluhu Hassan

Na Mara Online News
---------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa kumfanyia mambo mawili makuu, kwa manufaa ya wananchi.

Ametaja jambo la kwanza kuwa ni kusimamia vizuri mapato na matumizi ya fedha za Serikali, na la pili ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma nzuri za kijamii.

Rais Samia amesisitiza hayo wakati wa hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Mikoa tisa na Makatibu Tawala wa Mikoa kadhaa, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam leo Agosti 1, 2022.

“Sina msalia mtume kwenye mapato na matumizi… kuna fedha nyingi zinashushwa huko chini ili kusukuma miradi kwa wananchi,” amesema kiongozi huyo wa nchi.

Amewasisitiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kuwa fedha za Serikali zinazopelekwa kwenye maeneo yao ya uongozi zinatekeleza miradi ya kijamii kama vile maji, afya, elimu na barabara kama ilivyokusudiwa.

Kuhusu huduma kwa wananchi, amewaagiza Wakuu wa Mikoa akisema “Nendeni mkawahudumie wananchi kwa moyo safi, na mkifanya vizuri mtanyanyuliwa.”

Aidha, Rais Samia amewataka viongozi hao kutoruhusu mivutano ya matumizi ya fedha za umma na kuchelewesha huduma kwa wananchi.

Sambamba na hilo, amewakumbusha Wakuu wa Mikoa kutambua kuwa ni wawakilishi wake kwa wananchi mikoani, hivyo waepuke kuwabagua katika misingi ya urafiki na uadui, bali wawathamini na kuwahudumia kwa usawa.

Rais Samia ametumia nafasi hiyo pia kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine kutowanyima wananchi haki ya kuonesha mabango ya malalamiko yao kwa viongozi wa juu wanaotembelea maeneo yao.

“Nilisem sitaki kuona mabango maana yake [viongozi wenye dhamana] mfanye kazi vizuri. Mkifanya kazi vizuri maana yake hakuna malalamiko.

“Mabango ya malalamiko maana yake hamfanyi kazi yenu vizuri. Mwananchi akija na mabango ndiyo mdomo wake wa kulalamika,” amesisitiza Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia amewapongeza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wapya, akisema amewateua kwa kuangalia sifa za uwezo wao wa kazi, uaminifu wao kwa Serikali na imani yake kwao - kwamba wanaweza kumsaidia kuwatumikia wananchi ipasavyo.

Amewatakia heri katika majukumu yao ya kiserikali na kuweka wazi kuwa atafuatilia utendaji kazi wao.

“Hongereni sana, karibuni kazini, kazi iendelee,” Rais Samia amewambia viongozi hao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages