Dkt Philip Mpango
Na Sauti ya Mara Digital
------------------------------
SHIRIKA la ATFGM Masanga limeeleza kufarijika na kauli ya Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango ya kuwataka wananchi kukemea ndoa na mimba za utotoni.
“Ukiona viongozi wa juu wanakemea jambo hilo hadharani, kwetu sisi ni faraja kubwa sana,” alisema Meneja Mradi wa shirika hilo, Valerian Mgani katika mazungumzo na Sauti ya Mara Digital wilayani Tarime, juzi.
Mgani amesema ingawa Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo akiwa Mpanda mkoani Katavi, itaweka msukumo wa kukemea ndoa na mimba za utotoni nchini kote.
“Hakika tumefurahi kuona na kusikia kwamba viongozi wa juu wako upande wetu, na pengine viongozi wa ngazi nyingine za juu waliongelee na kulikemea jambo hilo ili kuleta mwamko zaidi kwa jamii,” amesema Mgani.
ATFGM Masanga ni shirika ambalo limejikita katika utoaji wa elimu ya madhara ya ukatili na unyanyasaji, ikiwemo ukeketaji, vipigo, mimba na ndoa za utotoni.
Hivi karibuni, Makamu wa Rais Dkt Mpango akiwa Mpanda aliwataka wananchi kuwa mstari wa mbele kukemea ndoa na mimba katika umri mdogo.
Alisema mimba za utotoni zina madhara makubwa ikiwemo kifo na maradhi ya fistula.
No comments:
Post a Comment