Na Mara Online News
--------------------------------
BENKI ya NMB imetoa msaada wa mabati 600 yenye thamani ya shilingi milioni 24 kwa ajili ya kuezeka majengo ya shule za msingi Gamasara, Ntaburo, Kimairi na Nyamwino katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara.
Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus amekabidhi msaada huo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo na viongozi wa elimu katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Gamasara, leo Septemba 22, 2022.
“Sisi kama Benki ya NMB inayoongoza Tanzania tuna wajibu wa kuunga Serikali mkono katika kusaidia jamii ya Watanzania, wakiwemo wanaotumia huduma zetu za kibenki, na kwetu sekta ya elimu ni jambo la kipaumbele,” amesema Ladislaus aliyefuatana na Meneja wa NMB Tawi la Tarime, Victorine Kimario katika makabidhiano hyo.
Kwa mujibu wa Meneja Ladislaus, msaada huo ni mwendelezo wa ushiriki wa benki hiyo katika maendeleo ya nchi kwa kurudisha kwa jamii sehemu ya faida wanayopata.
“Tumekuwa tukitoa msaada wa madawati na mabati kwa ajili ya shule, na sasa tumeanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa chuo kikuu. Na kwenye sekta ya afya tunatoa vitanda, magodoro na vifaa vya kuezekea,” ameongeza.
Meneja Ladislaus (aliyesimama) akizungumza katika hafla hiyo. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya, Kanali Mntenjele, wa tatu kutoka kulia ni Mkurugenzi Gimbana na viongozi wengine.
Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya, Kanali Mntenjele, ameishukuru Benki ya NMB akisema msaada huo utapunguza mahitaji ya mabati ya kuezeka majengo ya shule hizo.
“Bado tutaendelea kuthamini mchango unaotolewa na Benki ya NMB, mashirika, kampuni na taasisi nyingine katika kuchangia maendeleo ya kijamii ndani ya wilaya yetu,” amesema Kanali Mntenjele.
Naye Afisa Elimu ya Awali na Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mwalimu Matiko Kebaha ameishukuru benki hiyo, akisema msaada wa mabati hayo utanufaisha wanafunzi 720 kutokana na majengo yatakayoezekwa katika shule hizo.
No comments:
Post a Comment